Kampeni ya upandaji miti Jiji la Dodoma yafanikiwa S/M Mbwanga

Na. Mwandishi Wetu, DODOMA

Jiji la Dodoma limeendelea kutekeleza kampeni ya upandaji miti ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Zoezi hilo limefanyika katika maeneo mbalimbali ya jiji ikiwemo shule, taasisi za umma, barabara na maeneo ya makazi.


Akizungumza katika Shule ya Msingi Mbwanga, Katibu Tawala wa Wilaya ya Dodoma, Sakina Mbugi alisema kuwa zoezi la upandaji miti ni muendelezo wa kulifanya Jiji la Dodoma kuwa la kijani na pia kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika siku yake ya kuzaliwa.

Aliwataka wanafunzi, walimu na wananchi kwa ujumla kujenga utamaduni wa kupanda na kutunza miti ili kulinda mazingira na kuhakikisha ustawi wa vizazi vijavyo. Alisisitiza kuwa upandaji wa miti shuleni una mchango mkubwa katika kuelimisha watoto kuhusu umuhimu wa mazingira tangu wakiwa wadogo. "Tunapanda miti hii kwasababu ya kuungana na Mhe. Rais, Dkt. Samia kumpongeza katika siku yake ya kuzaliwa, ardhi hii itatunzwa na kuwa imara kama mtaungana katika usimamizi mzuri wa miti tuliyopanda leo. Tunayo Dodoma moja na inatutegemea sisi, kumbukeni jambo tulilofanya leo ni muhimu sana kwasababu miti hii itatufaidisha sisi wenyewe. Pia itasaidia kuondokana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko na mmomonyoko wa ardhi" alisema Mbugi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mnadani, Mugendi Kerenge, aliwataka wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira kwa kupanda na kutunza miti. Alisema kuwa wananchi wanapaswa kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kuwa ni jukumu la kila mmoja na sio serikali pekee. “Ni muhimu kupanda miti na ni wajibu kuitunza hadi ikue. Hii italinda ardhi yetu, kuleta mvua za uhakika na kuboresha maisha ya vizazi vijavyo” alisema Kerenge.

Zoezi hilo lilishirikisha viongozi wa serikali ya mtaa, wanafunzi, na wanachi ambapo jumla ya miti 150 ilipandwa shuleni hapo. Wadau wote walioshiriki waendelee kuhakikisha kuwa zoezi la upandaji miti linafanyika mara kwa mara ili Dodoma ibadilike kimazingira kwa miaka ijayo.

















 

Comments

Popular Posts

SERIKALI YAPONGEZWA KUTOA FEDHA UJENZI WA DODOMA ENGLISH MEDIUM

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma

Nanenane ni muhimu kujifunza Kilimo na Ufugaji bora