Hospitali ya Jiji la Dodoma mkombozi kwa wananchi wa Kata ya Nala
Na. Leah Mabalwe, NALA
Mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Jiji la Dodoma, uliopo
katika Kata ya Nala umegharimu kiasi cha shilingi 1,000,000,000 umekamilika na
umeanza kutumika ukiwanufaisha wananchi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Diwani wa Kata ya Nala, Herman Masila alisema kuwa hospitali hiyo ni msaada mkubwa kwa wananchi. “Kipekee nitoe pongezi kwa serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuboresha sekta ya afya katika kata yetu ya Nala. Serikali imetupendelea sana kwa kutujengea hospitali kubwa na ya kisasa zaidi kwaajili ya wananchi wa Kata ya Nala na kata jirani wanaweza kupata huduma katika hospitali hii. Ni kweli wananchi tayari wameshaanza kupata huduma katika hospitali yetu na tunanufaika nayo” alisema Masila.
Nea, Marry Kaka mwananchi wa Kata ya Nala akaishukuru
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utekelezaji wa mradi wa
Hospitali ya Jiji la Dodoma. “Tunaishukurun sana serikali chini ya Rais, Samia,
kwa kutujengea Hospitali ya Jiji kwenye kata yetu. Hospitali hii inaenda kuwa
mkombozi kwa wananchi wa Nala na maeneo jirani kwani hapo zamani tulikua
tunatembea umbali mrefu kufuata huduma za afya, lakini baada ya Hospitali hii
kujengwa kwasasa tunapata huduma karibu na kwa wakati” alimalizia Kaka.
Kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, kiasi cha shilingi
400,000,000 kimetengwa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi, ambapo tayari shilingi
366,676,122.59 zimetumika huku shilingi 33,323,877.41 zikiwa hazijatumika. Ununuzi
wa samani kwa jengo la wagonjwa wa nje ‘OPD’ umetumia shilingi 20,000,000 na
mchakato wa manunuzi unaendelea. Vifaa vya kuzalisha na kusaidia watoto njiti
vimenunuliwa kwa shilingi 18,135,000 lakini bado havijafungwa kutokana na
kutokuwepo kwa wazabuni.
MWISHO
Comments
Post a Comment