Sekta ya Michezo yaguswa Bajeti 2025/2026 Halmashauri ya Jiji la Dodoma
Na. Mussa Richard, DODOMA
Halmashauri ya Jiji la
Dodoma imepanga kujenga viwanja vya michezo ikiwemo uwanja wa mpira wa miguu uliopo
katika mchakato wa ujenzi, kuelekea michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027
ambapo kwa pamoja nchi za Afrika Mashariki Tanzania, Kenya na Uganda zitakuwa
wenyeji wa michuano hiyo.
Mpango huo umewekwa wazi
na Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma Francis Kaunda kwa niaba ya
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Dkt.
Frederick Sagamiko, wakati akiwasilisha Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026
katika Baraza Maalum la Madiwani, lililofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa
Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Kwa upande wake Daudi
Fundikira, Diwani wa Kata ya Chang'ombe baada ya kupitishwa kwa Bajeti hiyo
alisema "Tumepanga kujenga viwanja vya michezo katika Halmashauri ya Jiji
la Dodoma ambavyo vitakua ni sehemu ya kuongeza mapato kwa jiji letu la Dodoma,
lakini pia ni fursa kwa vijana wetu kufanya mazoezi na kuweza kuonekana, kwani
michezo ni ajira na michezo ni burudani”
Aidha, Diwani wa Kata ya
Chamwino, Jumanne Ngede, alielezea faida za ujenzi wa viwanja hivyo katika Halmashauri
ya Jiji la Dodoma na kwa jamii kiujumla. "Kwanza nimpongeze sana Mkurugenzi
wa Jiji la Dodoma Dkt. Frederick Sagamiko na timu yake kwa mpango huu mzuri wa
ujenzi wa viwanja, kwasababu faida zake si kwa Halmashauri tu kuingiza kipato,
bali hata kwa wananchi, mfano wafanyabiashara wadogo wataweza kufanya biashara
zao na kupata wateja zaidi kutokana na muingiliano wa watu utakao kuwa
unafanyika viwanjani". Alisema Ngede.
Kwa mujibu wa wasilisho la
Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Francis Kaunda alisema Mpango wa
Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni shilingi 147,910,202,949.46,
ikipanga kukusanya mapato ya ndani kiasi cha shilingi 67,385,000,000.00, ruzuku
za mishahara ikiwa ni shilingi 65,739,308,000.00 ruzuku ya matumizi mengine
ikiwa ni shilingi 3,071,349,000,00 na ruzuku ya miradi ya maendeleo ikiwa ni shilingi
11,714,545,949.46. Bajeti hiyo ikiongezeka kwa asilimia 7.04 kulinganisha na Bajeti
ya Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Comments
Post a Comment