Baraza la Madiwani Jiji la Dodoma lapitisha Bajeti 2025/2026 shilingi bil. 147
Na. Coletha Charles, DODOMA
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya
Jiji la Dodoma lapitisha kwa kauli moja rasimu ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa
Fedha 2025/2026 jumla ya shilingi bilioni 147.9 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.04
ukilinganisha na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi
wa mikutano wa halmashauri wa jiji hilo, ambao ulilenga kupitisha mapendekezo
ya rasimu ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026.
Akiwasilisha
rasimu hiyo, Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Francis Kaunda, alisema kuwa
halmashauri imekasimia
kukusanya shilingi bilioni 67.3 kati ya fedha hizo bilioni
43 ni mapato yasiyolindwa na shilingi 24.3 ni mapato lindwa, ambapo
halmashauri ipo kwenye kundi ambalo asilimia 70 ya mapato yasiyolindwa
inayoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo na asilimia 30 ni kwa ajili ya
matumizi ya kawaida.
Alisema kuwa, rasimu ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 itagharamiwa
na vyanzo vikuu vinne ikiwemo serikali kuu shilingi bilioni 68.9 kati
ya fedha hizo shilingi 68.8 (Mishahara na Matumizi ya kawaida)
na shilingi Bilioni 10 ni ununuzi wa vifaa tiba na dawa, Halmashauri
ya Jiji kupitia mapato ya ndani shilingi bilioni 67.3,
wahisani shilingi bilioni 11.7 na ubia (PPP) ambapo mwaka wa fedha
2025/2026, Halmashauri inategemea kuanza ujenzi wa Miradi mikubwa ambayo tayari
ilishafanyiwa usanifu na upembuzi yakinifu. “Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji,
naomba kuwasilisha rasimu ya makisio ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji
ya Dodoma kwa Mwaka wa Fedha 2025/26 kuwa ni jumla ya shilingi bilioni
147.9, kati ya fedha hizo shilingi bilioni 67.3 ni mapato ya
ndani, shilingi bilioni 65.7 ruzuku ya mishahara, shilingi
bilioni tatu (3) ruzuku ya matumizi mengineyo na
shilingi bilioni 11.7 ruzuku ya miradi ya maendeleo” alisema
Kaunda.
Akichangia mapendekezo ya rasimu ya Mpango
na Bajeti hiyo, Diwani wa Kata ya Viwandani, Jaffari Mwanyemba, alisema kuwa
bajeti hiyo ni kubwa ambayo itafanikisha miradi yote kutekelezwa na kuleta
maendeleo. Alishauri kuwa serikali iangalie kwa ukubwa eneo la stendi ya zamani
ya daladala, Jamatini kwa kufanyia maboresho kuepuka maswali kipindi cha
uchaguzi. “Bajeti ambayo imekuja mahali ambapo tunaihitaji na wananchi wetu
wanahitaji matokeo mazuri. Mama Samia mwaka 2024/2025 ametutendea haki
ametupatia fedha zaidi ya vile ambavyo tulitarajia hakika yote aliyofanya ni
utekelezaji wa ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi. Kwahiyo, mwezi wa kumi
tunakazi ya kufanya ili kuleta matokeo chanya.” alisema Mwanyemba.
Nae, Diwani wa Viti Maalum
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Anna Mng’ong’o, alisema kuwa bajeti ya mwaka huu
inaenda kujibu na kumaliza matatizo yote katika kata kulingana na fedha
iliyotengwa. “Huu mwaka ni mwaka wa uchaguzi, bajeti ni nzuri na imekidhi na
tunaenda kwa wananchi kujibu maswali kifua mbele kwa sababu tutakuwa tumefanya
mambo mazuri, tunampongeza mkurugenzi na jopo lake kwakweli wamefanya jambo
zuri sana” alisema Mng’ong’o.
Ikumbukwe
kuwa, katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, mambo mapya
yatakayofanyika ni pamoja na utekelezaji wa mradi wa kuongeza mnyororo wa
thamani kwa mazao ya zabibu na mboga mboga ambapo itahususha mashamba, ujenzi
wa kiwanda cha kuchakata zabibu eneo la Nala, kujenga ‘Park House’ kwa ajili ya
kuhifadhia zao la mbogamboga, ambapo kwa kiasi kikubwa itapunguza changamoto ya
soko la zabibu na wananchi watapata fursa ya kuuza mbogamboga kwenye masoko ya
ndani na nje ambapo kazi ya upembuzi yakinifu imeshaanza na inafanywa na TAHA
(Tanzania Holticuture Association) na uanzishaji wa mji wa kisasa Hombolo Bwawani
ambao utaunganishwa na mji wa Serikali Mtumba.
MWISHO
Comments
Post a Comment