Wananchi Dodoma wahimizwa kutunza Mazingira
Na. Aisha Ibrahim, DODOMA
Mkuu wa Kitengo cha Usafi na Udhibiti wa
taka ngumu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro, alisema kitengo kicho
kimejipanga kikamilifu katika kuendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za
udhibiti na uondoshaji wa taka ili kuhakikisha Jiji la Dodoma linakuwa katika
hali ya usafi na kuvutia.
Aliyasema hayo nje ya Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani la kupitia rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Akizungumzia kuhusu udhibiti wa taka
ngumu, Dickson Kimaro, alisema kupitia bajeti iliyotengwa na halmashauri,
kitengo hicho kinajiandaa na mchakato wa kununua mitambo maalum kwaajili ya
kuchakata takataka na kuwepo kwa gari ili kukusanya na kupeleka eneo la dampo
kuu la Chidaya. “Tunatarajia kwenda kununua mitambo ya kuchakata takataka, lakini
kununua malori kwaajili ya uondoshaji wa taka ili kuondokana na mfumo wa ‘Collection
Point’, bali kuchukua taka hizo na kupeleka dampo letu la Chidaya”, alisema
Kimaro.
Aidha, aliongeza kuwa katika bajeti hiyo
kutakuwa na ukusanyaji wa takwimu ya watumiaji na wazalishaji wa taka ili
kubaini kiwango cha uzalishaji wa taka hizo ikiwa ni njia mojawapo ya kuboresha
mfumo wa ukusanyaji na uondoshaji wa taka katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
“Tunakwenda kukusanya takwimu za watumiaji na wazalishaji wa taka, maeneo
walipo na kiwango wanachozalisha kwa lengo la kuboresha mfumo wa ukusanyaji na
uondoshaji wa taka katika jiji la Dodoma”, alisema Kimaro.
Nae, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani,
Prof. Davis Mwamfupe, alisema wananchi wanatakiwa kutunza mazingira kwa kupanda
miti ikiwa ni juhudi za kuunga mkono agenda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya utumiaji wa nishati safi ya kupikia. “Katika
kumuunga mkono mheshimwa Rais, katika adhima yake ya nishati safi tunahimizwa
utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti” alisema Prof. Mwamfupe.
Ukusanyaji na uhifadhi wa taka katika
maeneo maalum ni njia mojawapo ya kuhakikisha maeneo mbalimbali yanakuwa katika
hali ya usafi, pia kusaidia kuondokana na magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa
na uchafuzi wa mazingira.
MWISHO
Comments
Post a Comment