Baraza la Madiwani Jiji la Dodoma launga mkono maono ya Rais Dkt. Samia Nishati safi
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma inaunga mkono jitihada
zinazofanywa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha nishati safi kwa
wote inapatikana kwa lengo la kuboresha maisha ya watanzania.
Kauli hiyo ilitolewa na Mstahiki Meya wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe alipokuwa akifungua mkutano wa Baraza la
Madiwani kwa ajili ya kujadili na kupitia mapendekezo ya rasimu ya Mpango na Bajeti
kwa Mwaka wa Fedha 2025/ 2026 mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma.
Prof. Mwamfupe alisema “sisi Baraza la Madiwani la Halmashauri
ya Jiji la Dodoma tunatoa pongezi kwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa
kinara wa nishati safi. Mwanzo mwa wiki hii dunia yote macho yalikuwa Tanzania
kwa ajili ya mkutano wa nishati kwa ajili ya afya kwa manufaa ya wananchi wetu na mazingira bora. Dodoma ni wanufaika wakubwa wa dhana hiyo kwasababu miti
yetu itabaki salama. Sisi ni waungaji mkono namba moja wa dhana hii”.
Aliipongeza Timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji
la Dodoma na kusema kuwa mchakato ulikuwa shirikishi na umechukua nafasi yake.
Nafahamu mchakato ulipita katika vikao vyote vya kisheria kama Baraza la Wafanyakazi
la Jiji la Dodoma na Kamati ya Ushauri ya Wilaya. “Niwakumbushe tu kuwa
bajeti siyo mpango wa matumizi pekee, inahusu mpango wa mapato. Hivyo, tupo
hapa kujadili na kupitia mapendekezo ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2025/2026”
alisema Prof. Mwamfupe.
Awali akiwasilisha mapendekezo ya rasimu ya Mpango na Bajeti
kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu
Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Francis Kaunda alisema kuwa bajeti hiyo
imeongezeka kwa asilimia saba. “Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji naomba
kuwasilisha rasimu ya makisio ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la
Dodoma kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kuwa ni jumla ya shilingi 147,910,202,949.
Kati ya fedha hizo shilingi 67,385,000,000ni mapato ya ndani, shilingi
65,739,308,000 ruzuku ya mishahara, shilingi 3,071,349,000 ni ruzuku ya
matumizi mengineyo na shilingi 11,714,545,949 ruzuku ya miradi ya maendeleo.
Hivyo, bajeti imeongezeka kwa asilimia 7.04 ukilinganisha na bajeti ya mwaka wa
fedha 2024/2025” alisema Kaunda.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma
ilipitisha kwa kauli moja mapendekezo ya rasimu ya Mpango na Bajeti kwa mwaka
wa fedha 2025/2026 jumla ya shilingi 147,910,202,949.
MWISHO
Comments
Post a Comment