Sekta binafsi kugharamia miradi Jiji la Dodoma Bajeti ya 2025/2026
Na. Faraja Mbise, DODOMA
Sekta
binafsi itashiriki kugharamia miradi ya maendeleo kwa njia ya ubia katika
utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Halmashauri kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026
kutokana na umuhimu wa sekta hiyo kwa maendeleo ya Jiji la Dodoma.
Katibu wa Baraza la Madiwani, Dkt. Frederick Sagamiko
Mapendekezo
ya Rasimu ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 ya Halmashauri ya
Jiji la Dodoma, imeshirikisha sekta binafsi kutokana na matamanio na mahitaji
kuwa makubwa kuliko makusanyo ya mapato.
Hayo
yalisemwa na Katibu wa Baraza la Madiwani ambaye ni Mkurugenzi wa Jiji la
Dodoma, Dkt. Frederick Sagamiko, alipokuwa anatolea ufafanuzi katika baadhi ya
masuala yaliyowasilishwa katika Mkutano wa Baraza la Madiwani maalum kwa ajili
ya kupokea na kupitia mapendekezo ya rasimu ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha
2025/26 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma tarehe 30
Januari, 2025.
Dkt.
Sagamiko alisema “matamanio yetu na mahitaji yetu ni makubwa kuliko
makusanyo yetu ndio maana kwenye bajeti hii kipekee kabisa tunaweza
kushirikisha sekta binafsi katika ugharamiaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa Fedha
2025/2026 ile tuliyoiita ubia ‘PPP”.
Akizungumzia
kuhusu utekelezaji wa Mpango na Bajeti hiyo, alisema kuwa, kuna miradi mingi ya
kuvutia ambayo itashawishi wawekezaji kushirikiana nao katika utekelezaji. “Ipo
miradi mingi ambayo ni ya kuvutia sana ambayo tunaamini kabisa itaongeza ‘appetite’
kwa wawekezaji kuja kushirikiana nasi katika utekelezaji wa Mpango na Bajeti
hii kama miradi ilivyoainishwa pale” alisema Dkt. Sagamiko.
Kuhusu
ukamilishaji wa miradi viporo, alisema kuwa, dhamira ya Halmashauri ya Jiji la
Dodoma kupitia bajeti hiyo itaenda kukamilisha miradi yote viporo. “Dhamira
yetu ni kwamba, bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 inaenda kukamilisha miradi
yote viporo, haijalishi mradi huo ulipelekewa fedha za Serikali Kuu lakini
haikutosha au ulianzishwa kwa nguvu za wananchi, tunahakikisha miradi yote
inaenda kuisha. Ile milioni 150 tunayoiongelea haiendi kugusa miradi viporo,
miradi viporo imetengewa shilingi bilioni 7.1” alisema Dkt. Sagamiko.
Sambamba
na hilo alisema kuwa wamelenga katika kusogeza huduma karibu na wananchi
ikiwemo za ardhi, vibali vya ujenzi, na huduma zote zinazopatikana ofisi kuu
ili wananchi wasiweze kufuata huduma hizo umbali mrefu.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma,
Prof. Davis Mwamfupe, alisema kuwa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 ya
Halmashauri ya Jiji la Dodoma inalenga kukamilisha miradi viporo katika jumla
ya kata 41 za halmashauri hiyo.
“Kwa
mwaka huu, Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambayo inafikia takribani shilingi
Bilioni 147 inalenga kwenda kukamilisha miradi viporo katika kata zetu 41.
Viporo ni miradi ambayo haikuisha kwa wakati kutokana na namna ya kuibuliwa na
sisi wenyewe na serikali kwa ujumla na viporo vingine kuibuliwa na wananchi
wenyewe. Kwahiyo tumetenga kiasi cha Bilioni 7.1 ili iweze kwenda kukamilisha
hivyo viporo” alisema Prof. Mwamfupe.
Nae,
Diwani wa Viti Maalum Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Wendo Kutusha alipongeza
wasilisho la bajeti lililotolewa kwa kutenga fedha kwa ajili ya umaliziaji wa
miradi viporo kwa Kata zote za Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Tumeona
kwamba bajeti hii imetenga kiasi cha shilingi Bilioni saba kwa ajili ya
kumalizia miradi yote viporo. Katika kata zetu kuna miradi ambayo ni ya
serikali na iliyoibuliwa na wananchi, miradi hiyo imekuwa ikitesa sana huko kwa
pesa kidogo, inaenda kwa ‘speed’ ndogo lakini bajeti yetu inaenda kujibu na
kumaliza matatizo yote” alipongeza Kutusha.
Vilevile,
Diwani wa Kata ya Mkonze, David Bochela, aliondoa dhana iliyokuwepo kwa muda
mrefu ya Jiji la Dodoma kutegemea mapato ya ardhi na alisema kupitia miradi
iliyowasilishwa, Jiji la Dodoma litaenda kukusanya mapato kwa wingi. “Ilidhaniwa
wakati fulani kwamba Jiji la Dodoma linategemea mapato ya ardhi lakini
tunakwenda kutoka huko kwenye picha ya viwanja, kupitia miradi mikubwa ya
utekelezaji jiji letu litakusanya mapato mengi na kwa maana hiyo tutakuwa na
mapato mengi” alisema Bochela.
MWISHO
Comments
Post a Comment