MADIWANI JIJI LA DODOMA WATAKIWA KUTATUA KERO ZA WANANCHI

Na. Mwandishi Wetu, DODOMA

Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma watakiwa kusikiliza kero za wananchi na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati ili kuimarisha maendeleo na ustawi wa jamii.



Hayo aliyasema Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri, wakati alipokuwa akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Alisema kuwa madiwani ni kiungo muhimu kati ya serikali na wananchi, hivyo wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yao. “Madiwani ni sauti ya wananchi. Ni muhimu msikilize kwa umakini kero zao na kuzitatua kwa wakati ili kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima na kuongeza imani ya wananchi kwa serikali yao” alisema Alhaji Shekimweri.

Aliongeza kuwa utekelezaji wa majukumu hayo unahitaji uwajibikaji, ushirikiano na ufuatiliaji wa karibu wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inaleta matokeo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Makole, Omary Omary, alisema kuwa madiwani wanaendelea kuchukua hatua madhubuti katika kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi pamoja na kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika kata zao. “Sisi madiwani tupo karibu na wananchi wetu kila wakati. Tumejipanga kuhakikisha tunasikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na wataalamu pamoja na kusimamia ipasavyo miradi yote ya maendeleo,” alisema Omary.


Mkutano huo wa Baraza la Madiwani umeendelea kuwa jukwaa muhimu la kujadili na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, huku viongozi wakihimizwa kuzingatia uwajibikaji na ushirikiano katika kuleta maendeleo endelevu katika Jiji la Dodoma.

 

Comments

Popular Posts

JIJI LA DODOMA LATOA VIWANJA 1,900 KWA WAFANYAKAZI

Sungura kitoweo cha gharama nafuu