Jiji la Dodoma lajipanga kung’ara kwa usafi, Bilioni tatu yatengwa kwaajili ya miundombinu ya taka
Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
Halmashauri ya Jiji
la Dodoma imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuboresha mazingira na afya
za wakazi wake baada ya kuweka mpango mkakati wa kutenga shilingi bilioni tatu katika bajeti mpya ya fedha ijayo kwa
ajili ya kuimarisha miundombinu ya ukusanyaji wa taka.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu mpango huo, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula alisema kuwa bajeti hiyo inalenga kulifanya Jiji la Dodoma kuwa miongoni mwa majiji safi nchini kwa kuweka mifumo rafiki na ya kisasa ya kushughulikia taka.
Alieleza kuwa fedha
hizo zinatokana na mapato ya ndani, jambo
linaloonesha uwezo wa jiji kujitegemea katika kugharamia miradi ya maendeleo.
“Suala la usafi wa mazingira halikwepeki na sisi tunasema kuwa haitawezekana
kuwa na jiji chafu. Kwenye bajeti yetu mpya tumetenga takribani shilingi
bilioni tatu kwaajili ya kuhakikisha vifaa vyote vya
kukusanyia taka vinapatikana”
alisema Chaula.
Katika utekelezaji
wake, jiji linatarajia kusambaza madastbini makubwa katika maeneo mbalimbali,
yatakayokuwa na mfumo wa utenganishaji wa taka. Hatua hiyo itarahisisha
ukusanyaji, usafirishaji na uchakataji wa taka, huku ikilenga pia kulinda
mazingira na kupunguza athari za kiafya kwa wananchi. “Mkakati
wetu ni kuhakikisha Jiji letu linakuwa safi muda wote. Hili linawezekana kwa
kuweka miundombinu bora na kwa kushirikiana na wananchi” alisisitiza Chaula.
Aidha, aliwataka
wananchi kuendelea kulipa kodi kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo ikiwemo usafi wa jiji, huku akiongeza kuwa mchango wa
wananchi kupitia kodi ndio msingi wa maboresho ya huduma wanazozipata kila
siku.
Mpango huo unatarajiwa
kuleta mageuzi makubwa katika usimamizi wa taka, kulifanya jiji kuwa na
mandhari safi, salama na linalovutia zaidi kwa wakazi na wageni.
MWISHO
Comments
Post a Comment