Zahanati ya Mpamaa yaboresha huduma Kata ya Miyuji
Na. Abdul Juma, MIYUJI
Wananchi
wa Mtaa wa Mpamaa, Kata ya Miyuji jijini Dodoma, wameeleza kufurahia kwao
maboresho makubwa yaliyofanywa na serikali katika Zahanati ya Mpamaa kuanzia
ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa vifaa tiba na usimikaji wa mfumo wa Tehama
yamerahisisha upatikanaji wa huduma na kuboresha mazingira ya kufanyika kazi.
Katika mahojiano na wanahabari waliotembelea zahanati hiyo kwa ajili ya kufuatilia maboresho yaliyofanywa katika zahanati hiyo wananchi walielezea kufurahia maboresho hayo na huduma zinazotolewa.
Mkazi wa
Mtaa wa Mpamaa, Anifa Sagika alisema kuwa anaishukuru serikali kwa kuwajengea
zahanati ya Mpamaa. “Hapo awali, tulikosa huduma muhimu, hasa sisi akina mama
wajawazito tulilazimika kutembea umbali mrefu au kujifungulia nyumbani. Sasa
tuna huduma inatolewa karibu nasi” alisema Sagika.
Nae Malimi
Charles alisema kuwa anapongeza juhudi za serikali kuhakikisha huduma za afya
zinapatikana katika kata hiyo. Alisema kuwa zahanati hiyo imesaidia kupunguza vifo
vya wajawazito na kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya na kumtaja Rais Samia
kuwa ametimiza ndoto ya muda mrefu ya wakazi wa Miyuji.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mpamaa, Happy Joshua, alieleza
namna mradi huo ulivyotekelezwa kwa mafanikio. “Ninamshukuru Rais, Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi yake. Pia nawashukuru Mbunge wetu wa Jimbo la
Dodoma Mjini, Anthony Mavunde, na Diwani wetu Beatrice Ngerangera kwa
kushirikiana kuleta maendeleo. Zahanati hii imesaidia sana, hasa kwa huduma za
mama na mtoto ambazo zamani zilifanyika chini ya mti katika kanisa la RC”
alisema Joshua.
Afisa
Tabibu na Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mpamaa, Dkt. Fatuma Maseli, alisema
kuwa zahanati hiyo ilipokea fedha Shilingi Milioni 43 kwa ajili ya ununuzi wa samani,
vifaa tiba, pamoja na kuwekewa mfumo wa kidigitali unaorahisisha utoaji wa
huduma. “Awali wagonjwa walikuwa wanakaa chini kwa kukosa viti, lakini sasa
tuna mazingira bora. Pia tumepatiwa kichomea taka hatarishi na mfumo wa kisasa
unaoitwa ‘Gothomis’. Tunawapongeza viongozi wetu na tunaomba Mungu azidi
kuwabariki,” alisema Dkt. Maseli.
MWISHO
Comments
Post a Comment