Kata ya Dodoma Makulu yanufaika na mkopo wa asilimia 10
Na. Abdul Juma, DODOMA MAKULU
Mkopo wa mapato ya ndani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma
usio na riba wa shilingi 328,800,000 umewawezesha wanawake, vijana na watu
wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi katika kata ya Dodoma Makulu.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Dodoma Makulu, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Sophia Abdallah alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu mikopo ya mapato ya ndani iliyokopeshwa kwa wanavikundi wa kata hiyo kwa kipindi cha serikali ya awamu ya sita.
Alisema kuwa serikali ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa kipindi cha miaka minne imewezesha vikundi vya wanawake 21, vikundi vya
vijana vitatu na vikundi vya watu wenye ulemavu sita kujikwamua kiuchumi na
kuboresha maisha yao. Alisema kuwa mikopo hiyo imekuwa fursa kwa vijana kufanya
biashara mbalimbali katika kata hiyo. “Baadhi ya vikundi vimeweza kununua
bajaji na pikipiki ili kufanya biashara ya usafirishaji wa abiria kutoka Chuo Kikuu
cha Dodoma kwenda Sabasaba. Eneo la marejesho, vikundi vimefanya vizuri
kurejesha kwasababu wamelipa kabla ya wakati kufika. Vikundi vingine vimeweza kuomba
tena mkopo kwa awamu hii inayotarajiwa kukopeshwa tena. Hivyo, nivipongeze
vikundi hivi na waendelee kuwa na juhudi zaidi” alipongeza Abdallah.
Kwa upande wake, mnufaika wa mkopo wa asilimia 10, Nazalena Kufakunoga alieleza namna mkopo ulivyoweza kumnufaisha katika shughuli zake za ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na kueleza alivyopata faida na kufungua duka linalouza bidhaa za matumizi ya nyumbani.
“Mkopo huu, tulichukua kwa kikundi
tukanunua ng’ombe, faida iliyopatikana tukafungua duka na sasa tunatarajia kuongeza
ng’ombe wengine. Naipongeza serikali kwa kuendelea kutuwezesha akina mama na makundi
mengine kwasababu zamani tulikuwa chini ila kwa sasa tumeinuka kiuchumi.
Tumeweza kujikwamua kwasababu tunasomesha watoto kupitia matokeo ya mkopo huu
wa asilimia 10” alieleza Kufakunoga.
MWISHO
Comments
Post a Comment