Wananchi washirikishwe katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo

Na. Dennis Gondwe, DODOMA

NAIBU Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Fadhili Chibago ametoa rai kuwa miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa wananchi washirikishwe kikamilifu ili wawe sehemu ya miradi hiyo na kusema kuwa utaratibu huo utaifanya miradi kudumu kwa muda mrefu.



Kauli hiyo aliitoa alipoongoza Kamati ya Fedha na Utawala timu namba tatu kutembelea na kukagua umaliziaji wa vyumba vitatu vya madarasa katika Shule ya Msingi Nguji iliyopo Kata ya Ng’hong’onha, jijini Dodoma.

Alisema kuwa halmashauri inatekeleza miradi mingi ya maendeleo. “Nitumie nafasi hii kuwasisitiza kuendelea kuwashirikisha wananchi wa eneo husika kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Wananchi wakishirikishwa wanakuwa wamiliki wa mradi husika. Wasiposhirikishwa wanajiona siyo sehemu ya mradi. Hata kama kuna mtu anataka kufanya uharibifu kwenye mradi, wananchi wanabaki wanamtazama kwa sababu hawajashirikishwa. Nitumie nafasi hii kutoa rai, kwenye miradi yetu tunapoitekeleza, tuwashirikishe wananchi kuanzia mwanzo wa mradi hadi utakapokamilika ili wao waone fedha wanazolipa kama kodi zinavyofanya kazi. Vilevile, niwashukuru wadau mbalimbali wanaosaidia kutoa fedha kuhakikisha miradi yetu inakamilika kwa wakati” alisema Chibago.



Shule ya Msingi Nguji ilipelekewa shilingi 21,000,000 kwa ajilia ya umaliziaji vyumba vitatu vya madarasa, ujenzi wa Ofisi ya Machinga Mkoa ilipelekewa shilingi 52,460,000 na ukamilishaji wa miundombinu na ujenzi wa mabweni mawili, vyumba vinne vya madarasa, matundu 10 ya vyoo na nyumba pacha ya walimu Shule ya Sekondari Miyuji B ilipelekewa shilingi 567,000,000.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Osterbay Dodoma wajitokeza usafi wa mazingira

Usafi wa Mazingira Kipaumbele Kata ya Chamwino

Wananchi wa Kata ya Mtumba wanufaika na Mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri