Shule mpya ya Kata, Sekondari Miyuji B yajengwa kisasa kutoa elimu bora
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KAMATI
ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imempongeza Rais, Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa nia yake njema ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma
bora hasa za elimu baada ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo yenye
zaidi ya shilingi 500,000,000 katika kata tatu za jiji hilo.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Fadhili Chibago alipoongoza timu namba tatu ya Kamati ya Fedha na Utawala kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika kipindi cha robo ya tatu ya Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Alisema
kuwa kamati yake ilitembelea kata tatu za Ng’hong’ohna, Makole na Miyuji
kukagua miradi ya maendeleo. “Leo tumekuwa na ziara nzuri ya kutembelea miradi
mbalimbali katika kata tatu za Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Kamati ya Fedha
na Utawala tuligawana na kupeana majukumu ya kutembelea miradi ya maendeleo.
Timu yangu tumekagua umaliziaji wa vyumba vitatu vya madarasa Shule ya Msingi
Nguji, Kata ya Ng’hong’onha, ujenzi wa Ofisi ya Machinga Mkoa wa Dodoma na
ukamilishaji wa miundombinu Shule ya Sekondari Miyuji B ulipo ujenzi wa mabweni
mawili, vyumba vinne vya madarasa, matundu 10 ya vyoo na nyumba pacha ya walimu”
alisema Naibu Meya Chibago.
Akiongelea
utekelezaji wa miradi hiyo alisema kuwa imetekelezwa kwa kiwango bora. “Kamati
tumejiridhisha kwamba fedha za serikali na walipa kodi zimetumika kwa usahihi.
Miradi yote imejengwa kwa kuzingatia vigezo vyote vinavyohitajika na ubora umezingatiwa.
Kwa niaba ya Kamati ya Fedha na Utawala ya Jiji la Dodoma, nimshukuru sana Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika nia yake
njema ya kuhakikisha wananchi wa Dodoma wanafikiwa na huduma zilizo bora.
Watoto wetu wasome katika madarasa mazuri, lakini pia wapate huduma nzuri
kutoka kwa walimu wao. Sisi Kamati ya Fedha na Utawala tutaendelea kumuunga
mkono katika kutekeleza majukumu yake” alisema Naibu Meya Chibago.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Miyuji B kwa Kamati ya Fedha na Utawala, Mkuu wa Shule hiyo, Mwl. Clara Mwinshehe alisema kuwa shule yake ilianza mwaka 2024 kutokana na fedha za Mradi wa Kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP). “Shule ilipokea shilingi 454,000,000 mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu. Nyumba pacha ya walimu shilingi 95,000,000, mabweni mawili shilingi 250,000,000, matundu 10 ya vyoo shilingi 17,000,000 na madarasa manne shilingi 92,000,000. Kati ya fedha hizo kiasi kilichotumika ni shilingi 340,000,000 na malipo mengine yapo kwenye utaratibu” alisema Mwl. Mwinshehe.
Katika
shule hiyohiyo, Halmashauri ya Jiji la Dodoma ilitoa kiasi cha shilingi
113,000,000 fedha kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya umaliziaji na ukarabati
ya jengo la TEHAMA, maktaba, madarasa matatu, choo matundu 10, maabara tatu za
Fizikia, Kemia na Baiolojia pamoja na gharama ya kuunganisha umeme kwenye
majengo yote.
Shule
ya Sekondari Miyuji B ni shule ya kata iliyoanzishwa mwaka 2024, ina wanafunzi
208, wanafunzi wa Kadato cha Pili 163 na Kidato cha Kwanza walioripoti ni 80.
MWISHO
Comments
Post a Comment