Jengo jumuishi la kutolea huduma za Afya Makole lipo katika hatua nzuri ya ujenzi
Na. Nancy Kivuyo, MAKOLE
Mradi wa ujenzi wa jengo jumuishi
la kutolea huduma za afya katika Kituo cha Afya Makole wenye zaidi ya shilingi
bilioni moja lipo katika hatua nzuri ya utekelezaji wake.
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makole, Dkt. Salma Gwassa alipokuwa akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Makole kwa Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma iliyotembelea maendeleo ya mradi huo.
Alisema kuwa kiasi cha
shilingi 750,000,000 kimetolewa na serikali kuu na fedha za mapato ya ndani ya
Halmashauri ya Jiji la Dodoma shilingi 289,794,329 zimelipwa kwa mkandarasi
kwaajili ya ujenzi huo.
Alisema kuwa ujenzi upo
katika hatua ya msingi na wanatarajia mradi utakapokamilika wananchi wa Kata ya
Viwandani na Jiji la Dodoma kwa ujumla watapata matibabu hapo. “Mradi huu
ukikamilika huduma za kliniki za kibingwa ‘speciality clinic’ zitapatikana, huduma
za kiutawala zitaboreka na tutapanua wigo wa utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa
nje na wa ndani” alisema Dkt. Gwassa.
Nae, Msimamizi wa mradi,
Mhandisi Ntezimana Chongele alisema kuwa mradi upo katika hatua nzuri na
utatekelezeka kwa wakati. “Napenda kuwahakikishia kuwa mkandarasi yupo vizuri,
eneo hili lina asili ya maji kama mnavyoona amefanya kazi kubwa kuyavuta na
anatarajia kuendelea na ujenzi kwa kasi kuhakikisha anamaliza mradi ndani ya
muda uliopangwa” alisema Mhandisi Chongele.
Kwa upande mwingine
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya Jiji la Dodoma, Joan Mazanda
aliisisitiza kamati ya mradi kusimamia vizuri mradi huo ili ukamilike kwa
wakati wananchi wapate huduma za matibabu. “Kituo cha Afya Makole kinatoa
huduma za afya nzuri sana, tunategemea ujenzi ukikamilika wananchi watapata
huduma nzuri. Nawasisitiza kusimamia vilivyo mradi huu, fedha iliyotolewa ni
nyingi tutafurahi kuona unakamilika kwa viwango vile tunavyotarajia”
alisisitiza Mazanda.
Mradi wa ujenzi wa jengo
jumuishi la kutolea huduma za afya Kituo cha Afya Makole unatarajiwa kukamilika
tarehe 27 Januari, 2026 na unatarajia kuhudumia wananchi 95,320 kwa mwaka.
MWISHO
Comments
Post a Comment