Ujenzi wa Darasa Sekondari Anthony Mavunde kupunguza msongamano kwa wanafunzi
Na. Nancy Kivuyo, HOMBOLO BWAWANI
Mkuu
wa Shule ya Sekondari Anthony Mavunde, Mwalimu Emmanuel Magumba amesema kuwa
shule hiyo ilipokea kiasi cha shilingi 15,425,000 kwa ajili ya ujenzi wa darasa
moja na ununuzi wa viti 50 na meza 50 kwa lengo la kuongeza miundombinu katika
shule hiyo.
Mwl. Magumba alisoma taarifa ya mradi huo mbele ya Kamati ya Fedha na Utawala ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kusema kuwa pamoja na ujenzi unaoendelea anaiomba halmashauri iwaongezee fedha kwa ajili ya kumalizia darasa hilo. “Hatua tuliyofikia ni nzuri kwasababu umaliziaji darasa hili sio mkubwa kama unavyoanza ujenzi” alisema Mwl. Magumba.
Aliongeza
kuwa kukamilika kwa darasa hilo kutaleta chachu ya wanafunzi kusoma kwa bidii. “Mheshimiwa
Mwenyekiti, mradi wa ujenzi wa darasa hili ukikamilika naamini wanafunzi wetu
watapata nafasi ya kusoma na wataongeza bidii katika masomo” aliongeza Mwl.
Magumba.
Nae, Mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza, Emmanuel Mbega alisema kuwa anaishukuru serikali kwa kuwajengea shule karibu. “Napenda kutoa shukrani kwa serikali kwa kutujali sisi wanafunzi. Kiukweli uwepo wa Sekondari ya Anthony Mavunde umetupunguzia adha ya kwenda mbali kusoma” alishukuru Mbega.
Kwa
upande mwingine Mwanafunzi wa Kidato cha Pili, Salma Malima alisema kuwa uwepo
wa sekondari hiyo umeondoa adha ya kutembea umbali wa kilomita nane kufuata
shule Hombolo. ”Tunashukuru sana kuwepo shule hii hapa, kwanza imetusaidia
kupunguza umbali wa kutembea kwenda shuleni. Lakini imetusaidia sisi wanafunzi
wa kike kuepukana na vishawishi vya barabarani. Wapo wenzetu walipata mimba za
utotoni sababu ya mazingira magumu ya kufika shuleni. Nina furaha sana kusoma
hapa sasa” alishukuru Malima.
MWISHO
Comments
Post a Comment