DC Shekimweri awaasa viongozi kutokuchukulia mzaha suala la madada poa

Na. Shahanazi Subeti, DODOMA

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri, alitoa maoni kwa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma kufanya utafiti, kutoa elimu na kuweza kujua sababu zinazowafanya wanawake na vijana kufanya biashara ya ngono.


Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir Shekimweri

Aliyasema hayo wakati wa Mkutano wa Baraza la Madiwani kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa kazi robo ya pili kwa kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Desemba, 2025 uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Alhaji Jabir Shekimweri alisema “Halmashauri ya Jiji la Dodoma ina mifuko mahsusi ya vijana na wanawake, hivyo uchunguzi ufanyike kujua kwanini matendo ya uzinifu yanaendelea. Katika kutafuta suluhisho pengine Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani, ingawa taarifa ilipitishwa sioni kama vita ya biashara hiyo ya watu kujiuza katika shughuli za ngono haihitaji ‘cohesive force’ nguvu ya dola, nadhani inahitaji elimu zaidi na mikakati ya kuwafikia hao na pengine kuwabadilisha”.

Pia, aliwaasa viongozi kutokuchukulia rahisi suala hili “kwenye kamati ya usalama tumechukuwa hatua mfano Msikiti wa Gadafi tumewahi kufanya oparesheni pale kwenye ile ‘Guest’ inaitwa 'Msangi' na tumefanikiwa kukamata watu kwa mara moja karibu 14 ni jambo la kadhia sana. Fikiria unafanyika ufuska nyuma ya msikiti wengine wanaitwa wafanye ibada na wengine wanafanya uzinifu. Kwahiyo suala la kufanyiwa mzaha sio zuri, eneo la area 'C' na area 'A' pia tumefanya oparesheni na tumewakamata hao watu” alisema Alhaj Shekimweri.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya  Ihumwa,vEdward Magawa, alisema kuna mipango ambayo ni madhubuti iliyowekwa katika kata yake ili kutokomeza tabia mbaya inayoleta mmomonyoko wa maadili katika Jiji la Dodoma. “Biashara hii kwa Dodoma imeshamiri sana, sio katikati ya mji hata pembezoni mwa mji kwenye kata kama Ihumwa. Lakini pia Kuna mikakati mikubwa katika kata yangu ambayo tumeanza kuifanyia kazi na tumewatambua hao watu na kukaa nao kuona changamoto zao mpaka wanajiingiza kwenye hiyo biashara. Kwahiyo, katika mipango yetu tumewapa kipaumbele katika vikundi vya ujasiriamali, tunaona kwamba hawa ni watu ambao tunaweza kuwaweka na kuwakusanya ili kuanza biashara za ujasiriamali badala ya kuendelea na biashara hiyo. Kwakweli ni mmomonyoko wa maadili” alisema Magawa.

Nae Diwani wa Kata ya Makole, Omary Haji, aliwashauri kamati husika na viongozi wake kutokuchoka na kuweka mikakati mizuri katika kutokomeza suala hilo. “Kamati ya UKIMWI inapaswa kuweza kuona namna gani inaweza kuwatafuta wale watu kwa kukaa nao na kuwapa elimu ili kuondoa jambo hili. Katika vitendo hivi hawa wote wanaokuja kufanya hii biashara sio wenyeji wa Dodoma ni watu kutoka mikoa ya mbali na Dodoma” alisema Haji.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Mbunge Mavunde akabidhi Kompyuta kwa Kata 41 za Jiji la Dodoma

Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Majengo Dodoma watarajia makubwa Mradi wa TACTIC

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma