DC Shekimweri awaasa viongozi kutokuchukulia mzaha suala la madada poa
Na. Shahanazi Subeti, DODOMA
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaji Jabir
Shekimweri, alitoa maoni kwa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la
Dodoma kufanya utafiti, kutoa elimu na kuweza kujua sababu zinazowafanya
wanawake na vijana kufanya biashara ya ngono.
Aliyasema hayo wakati wa Mkutano wa
Baraza la Madiwani kwa ajili ya kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa
kazi robo ya pili kwa kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Desemba, 2025 uliofanyika katika
ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Alhaji Jabir Shekimweri alisema “Halmashauri
ya Jiji la Dodoma ina mifuko mahsusi ya vijana na wanawake, hivyo uchunguzi
ufanyike kujua kwanini matendo ya uzinifu yanaendelea. Katika kutafuta
suluhisho pengine Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani, ingawa taarifa ilipitishwa
sioni kama vita ya biashara hiyo ya watu kujiuza katika shughuli za ngono haihitaji
‘cohesive force’ nguvu ya dola, nadhani inahitaji elimu zaidi na mikakati ya
kuwafikia hao na pengine kuwabadilisha”.
Pia, aliwaasa viongozi kutokuchukulia
rahisi suala hili “kwenye kamati ya usalama tumechukuwa hatua mfano Msikiti wa Gadafi
tumewahi kufanya oparesheni pale kwenye ile ‘Guest’ inaitwa 'Msangi' na
tumefanikiwa kukamata watu kwa mara moja karibu 14 ni jambo la kadhia sana.
Fikiria unafanyika ufuska nyuma ya msikiti wengine wanaitwa wafanye ibada na
wengine wanafanya uzinifu. Kwahiyo suala la kufanyiwa mzaha sio zuri, eneo la
area 'C' na area 'A' pia tumefanya oparesheni na tumewakamata hao watu” alisema
Alhaj Shekimweri.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ihumwa,vEdward Magawa, alisema kuna mipango
ambayo ni madhubuti iliyowekwa katika kata yake ili kutokomeza tabia mbaya
inayoleta mmomonyoko wa maadili katika Jiji la Dodoma. “Biashara hii kwa Dodoma
imeshamiri sana, sio katikati ya mji hata pembezoni mwa mji kwenye kata kama Ihumwa.
Lakini pia Kuna mikakati mikubwa katika kata yangu ambayo tumeanza kuifanyia
kazi na tumewatambua hao watu na kukaa nao kuona changamoto zao mpaka
wanajiingiza kwenye hiyo biashara. Kwahiyo, katika mipango yetu tumewapa
kipaumbele katika vikundi vya ujasiriamali, tunaona kwamba hawa ni watu ambao
tunaweza kuwaweka na kuwakusanya ili kuanza biashara za ujasiriamali badala ya
kuendelea na biashara hiyo. Kwakweli ni mmomonyoko wa maadili” alisema Magawa.
Nae Diwani wa Kata ya Makole, Omary
Haji, aliwashauri kamati husika na viongozi wake kutokuchoka na kuweka mikakati
mizuri katika kutokomeza suala hilo. “Kamati ya UKIMWI inapaswa kuweza kuona
namna gani inaweza kuwatafuta wale watu kwa kukaa nao na kuwapa elimu ili
kuondoa jambo hili. Katika vitendo hivi hawa wote wanaokuja kufanya hii
biashara sio wenyeji wa Dodoma ni watu kutoka mikoa ya mbali na Dodoma” alisema
Haji.
MWISHO
Comments
Post a Comment