Wananchi Dodoma watakiwa kuzingatia vibali vya ujenzi
Na. Halima Majidi, VIWANDANI
Wananchi jijini Dodoma wametakiwa kuacha tabia ya ujenzi wa aina yoyote bila ya kufuatilia vibali kwa sababu ni kosa la kisheria na linaweza kusababisha ujenzi holela na migogoro ya Ardhi isiyo ya lazima.
Hayo yalisemwa na Msanifu Majengo wa Halmashauri ya
Jiji la Dodoma, Paschal Mathew wakati akitoa elimu juu ya umuhimu wa vibali vya
ujenzi kwa wananchi wanaotaka kujenga ikiwa ni muendelezo wa Kliniki ya Ardhi
inayofanyika jijini hapo katika viwanja vya iliyokuwa Manispaa ya zamani.
Alisema kuwa vibali vya ujenzi wanatoa kwa mujibu wa
sheria, na kwa viwanja vyote ambavyo vimeshafanyiwa vipimo na kumilikishwa ili
mwananchi apewe huduma, lazima awe na nyaraka za umiliki pamoja na michoro ya
majengo anayotaka kuendeleza yakizingatia matumizi na sheria ndogo za Halmashauri
ya Jiji la Dodoma. “Tunakagua michoro kuangalia kama imekamilika na imekidhi
vigezo vya kihandisi na kisanifu na kuwaandikia “invoice” kwaajili ya kufanya malipo
ya kibali cha ujenzi. Baada ya kulipia wataalamu watapitia michoro na kibali
chake kwa lengo la kujiridhisha” alisema Mathew.
Aidha, alifafanua kuwa muamko wa wananchi ni mkubwa
ila kuna changamoto ya uelewa, kuna mwingine anakuja kuomba kibali akiwa na
nyaraka ila hana michoro ya ujenzi. “Tunampa elimu kwanza ya namna gani afanye,
awasiliane na wataalamu wa aina gani ili aweze kuandaliwa michoro yake kisha
aje na michoro hiyo ili tuweze kumpa kibali. Mpaka leo tarehe 26 Februari tumepokea
zaidi ya maombi ya vibali vya uendelezaji
ujenzi 20, ambapo bado tunaendelea na huduma hiyo” alifafanua Mathew.
Nae, Epimark Madole ambae ni mkazi wa eneo la Mipango alipongeza
huduma za utoaji wa vibali, kwa sababu inasaidia kujenga katika sehemu husika
na kuepusha migogoro na Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Tunapaswa kuzingatia
taratibu zote za jiji kuhusiana na vibali vya ujenzi, usijenge kabla ya kuomba
kibali cha ujenzi, unatakiwa ufuate taratibu ikiwemo kuwa na michoro iliyokaguliwa
na kulipia ili kuepuka malumbano na Jiji la Dodoma” alisema Madole.
Sanjari na hayo alisema kuwa mtu akijenga bila kupata
kibali anaweza kujenga sehemu ambayo sio rasmi ikiwemo barabarani kwa sababu anakuwa
hajazingatia mipaka. “Unaweza ukajenga eneo ambalo lilitakiwa kujengwa makazi wewe
ukajenga ‘commercial’ au maduka. Kwa hiyo, lazima kuzingatia kwa kufuata sheria
ili kuepusha usumbufu wa kubomolewa majengo yetu” alisema Madole.
Kwa upande wake Fausta Kusakala alisema kuwa changamoto
yake ni kiwanja chake kilichopo Chinangali West ambapo kila akiingia kwenye
mtandao anaambiwa kiwanja kimefutwa. “Kwa ujumla huduma ni nzuri, nimeambiwa
niende kwa Kamishna kwaajili ya hitimisho” alisema Kusakala.
MWISHO
Comments
Post a Comment