Dodoma Jiji FC inafukuza Mwizi Kimya Kimya

Na. Mussa Richard, DODOMA

Timu ya Soka ya Dodoma Jiji FC, imeendelea na maandalizi ya kujiwinda na michezo ya Ligi kuu ya NBC Tanzania bara, kwasasa imekita kambi mkoani Arusha, na imecheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza Mbuni FC, mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha na Dodoma Jiji FC kuchomoza na ushindi wa bao 1-0.




Akizungumza baada ya mchezo kutamatika Kocha wa Viungo wa Dodoma Jiji FC, Fransis Mkanula alisema “tumekuja hapa Arusha kuweka kambi ya siku tano, tumekuja hapa kupata mechi za kirafiki kwasababu timu imetoka kwenye mapumziko, baada ya ratiba kutoka tukaamua kuja hapa Arusha kucheza mechi za kirafiki ili kurudisha utimamu wa miili kwa wachezaji pia ukizingatia tuna maingizo mapya kwenye timu. Kwahiyo, tumekuja kutengeneza mazingira ya kuzoeana na wenzao na kuingia kwenye mfumo wa timu”.

Nae, Nahodha wa Dodoma Jiji FC, Augustin Nsata akaelezea hali ya kambi na maandalizi ya timu kuelekea kwenye michezo ya Ligi kuu ya NBC Tanzania Bara. “Hali ya kambi ni nzuri na hali ya hewa ya Arusha ni nzuri, tumekuja Arusha kwasababu kuna timu nzuri na zenye ushindani ambazo zitatupa kujua hali ya timu yetu. Kwasasa, jambo ambalo kwa mwalimu yeye anaona kama kuna madhaifu kwenye timu tukirudi uwanja wa mazoezi tukarekebishe ili kwenye mchezo wa kirafiki unaofuata tuweze kufanyia kazi maelekezo ya mwalimu”. alisema Nsata.

Mpaka sasa Dodoma Jiji FC imecheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar mchezo ulioisha kwa suluhu ya kufungana mabao 2-2, mchezo mwingine Dodoma Jiji FC, walishuka dimbani kuwakabiri Mbuni FC ambapo Dodoma Jiji FC ilishinda kwa bao 1-0, Dodoma Jiji FC imebakiza mchezo mmoja wa kirafiki ambao itacheza na timu ya Gunners FC.





MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma