Jiji la Dodoma kuingia ubia utekelezaji Miradi
Na. Halima Majidi, DODOMA
Halmashauri
ya Jiji la Dodoma katika kuhakikisha inaimarisha na kukuza wigo wa ukusanyaji
wa mapato kwa maendeleo yake na nchi kwa ujumla imeainisha miradi ya kuingia
ubia na kushirikisha sekta binafsi na za umma.
Akizungumza
katika Mkutano wa Baraza la Madiwani wa kupitia mapendekezo ya rasimu ya Mpango
na Bajeti ya Mwaka 2025/2026, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani, Prof. Davis Mwamfupe,
alisema kuwa halmashauri imekuja na mkakati mpya wa kujiweka tayari kwa kufanya
miradi kwa ubia kupitia mfumo wa ushirikishaji sekta binafsi na sekta ya umma (PPP).
Prof.
Mwamfupe alisema kuwa miradi mingi imewekwa katika masoko ili kuweza kuita na
kuvutia sekta binafsi ili waweze kushiriki na kuwekeza katika miradi hiyo. “Kwa
kuangalia miradi ambayo tulikuwa nayo kipindi cha nyuma na kwa kujifunza
kutokana na hiyo tumepata tabu sana kukamilisha miradi miwili ya hoteli. Kwahiyo,
tumeweka mkakati mpya wa kushirikisha sekta binafsi na za umma ili kurahisisha
ufanisi wa miradi hiyo”, alisema Prof. Mwamfupe.
Aidha,
Prof. Mwamfupe alisema kuwa wamefanikiwa kuanzisha kampuni Special Purpose Vehicle
(SPV) ambayo ni chombo cha kuendesha miradi ambayo inahusiana na biashara kwa
lengo la kutanua wigo wa mapato. Aliongeza kuwa “majukumu ya Halmashauri ya
Jiji la Dodoma si sana kufanya biashara. Lakini tunajikuta tunamiradi
inayofanya biashara ili kuondoa ukinzani wa namna hiyo tukasisitiza kuwa na
mfumo huo pale tunapokuwa na miradi ambayo inaingiza fedha. Pale tunapokuwa na
miradi ambayo ubunifu wake unahitaji utaalamu uliopo nje ya uwezo wetu ndio
maana tukaona SPV haikwepeki” alisema Prof. Mwamfupe.
Sambamba
na hilo, alisema kuwa serikali imeweka adhma ya kuanzisha mji katika eneo la
Hombolo Bwawani ikiwa ni katika muendelezo wa mipango miji wa 2019-2039. “Eneo
lile lina mandhari nzuri. Hivyo, kutenga maeneo na kujenga mji wa kisasa wenye
miundombinu bora na huduma muhimu kwa lengo la kuvutia wageni pamoja na kukuza
sekta ya utalii. Tunadhani masaki ya Dodoma itakuwa uekekeo wa namna hiyo”,
alisema Prof. Mwamfupe.
Kwa
upande wake Diwani wa Kata ya Makole, Omari Haji Omari, alisema anaupongeza
uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuweka mkakati wa ujenzi wa mji
mpya wa kipekee Hombolo Bwawani kwasababu sehemu hiyo itawasaidia watu kupata
mahitaji yao ya muhimu. “Mtu hatakuwa na sababu ya kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam
kwaajili ya kufurahi yaani 'kuenjoy' badala yake ataenda Hombolo Bwawani”
alisema Omari.
MWISHO
Comments
Post a Comment