Dodoma Jiji U20 FC yakamiwa na Maafande wa Gunners FC
Na. Mussa Richard, DODOMA
Timu ya soka ya Dodoma Jiji chini ya umri wa miaka 20
imechezea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Timu ya Gunners FC, katika mchezo wa
kirafiki uliovurumishwa katika uwanja wa Shell Complex jijini Dodoma hii leo.
Akizungumza baada ya kutamatika kwa dakika tisini Kocha
Mkuu wa Timu ya Dodoma Jiji U20, Jeremiah Chido alisema “mchezo umeisha salama,
tumepoteza mchezo kwasababu tumekutana na timu nzuri na yenye daraja la juu. Kwetu
sisi alikuwa ni mshindani sahihi kutokana na maandalizi yetu tunayoyafanya
kwaajili ya michezo inayofuata ya ligi ya vijana michezo ambayo tutakuwa
ugenini ndiyo maana leo tumewapa nafasi wachezaji wote ili kuwatengenezea
utimamu wa mwili kwaajili ya kurudi kwenye michezo ya ligi’’.
Katika hatua nyingine Chido akazungumzia hali ya
majeruhi kwenye timu yake na kuwaaminisha mashabiki kuwa wachezaji hao
watarejea uwanjani na kuendelea kuipambania timu. “Katika mchezo wa leo
wachezaji wawili wamepata majeraha, lakini siyo majeraha makubwa ya kuwaweka
nje kwa muda mrefu ni majeraha ya kawaida, tutashirikiana na madaktari kuhakikisha
afya zao zinaimarika haraka na wanarudi uwanjani kuja kuipambania nembo ya timu’’
alisema Chido.
Kwa upande wake Nahodha wa Dodoma Jiji U20, Bakari Mondwe
baada ya mchezo kuisha alisema “tumekutana na timu yenye uwezo mzuri wa
kiuchezaji kitimu na kwa mchezaji mmoja mmoja na ndiyo lilikuwa lengo letu
kupata timu yenye ushindani unaokaribiana na wapinzani tunaoenda kukabiriana
nao katika michezo inayofuata ya ligi tukiwa ugenini” alisema Mondwe.
Dodoma Jiji U2O FC, itajitupa tena dimbani Februari 12
katika uwanja wa Azam Complex itakapoikabiri Azam FC U20 katika mzunguko wa
kumi wa ligi kuu ya vijana ya NBC Youth League Tanzania bara.
MWISHO
Comments
Post a Comment