Kata 41 jijini Dodoma kunufaika na Milioni 150 za Miradi ya Maendeleo
Na. Shahanazi Subeti, DODOMA
Baraza la Madiwani wa Jiji la Dodoma wameipongeza
Halmashauri ya Jiji chini ya Mkurugenzi na jopo lake kwa kutenga shilingi bilioni
saba kwa ajili ya kumalizia miradi viporo na shilingi milioni 150 kwa kila kata
kuanzisha miradi mipya ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
Madiwani waliyasema hayo katika mkutano
maalum wa kupitia rasimu ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 uliofanyika
katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof.
Davis Mwamfupe, alisema kuwa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/2026 ya Halmashauri
ya Jiji la Dodoma inalenga kukamilisha miradi viporo katika jumla ya kata 41 za
halmashauri hiyo. “Kwa mwaka huu, Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma
inafikia takribani shilingi Bilioni 147 inayolenga kwenda kukamilisha miradi
viporo katika kata zetu 41. Miradi yote ambayo haikuisha kwa wakati kutokana na
sababu zozote zile. Hivyo, tayari imetengwa kiasi cha shilingi Bilioni saba ili
iweze kwenda kukamilisha hivyo viporo” alisema Prof. Mwamfupe.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kilimani,
Neema Mwaluko, alisema Mpango na Bajeti umekuwa ni mzuri sana na umelenga
kwenda kuwasaidia wananchi wa kawaida ili kuwanyanyua kiuchumi. “Tukiangalia
katika mpango huu na Bajeti, lengo mojawapo ni kumaliza viporo katika kata zetu.
Mpango na Bajeti hii umekuwa ni mpango rafiki sana kwa mazingira ya kutoa
huduma kwa wananchi wetu. Kwahiyo, naipongeza sana Timu ya Menejimenti ya Jiji
ikiongozwa na mkurugenzi na Baraza la Madiwani” alisema Mwaluko.
Nae, Diwani wa Viti Maalum, Anna Mng’ong’o,
alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa bajeti hiyo na
kusema kuwa itasaidia kutatua matatizo katika kata na kuleta maendeleo. “Bajeti
yetu ipo vizuri sana, bajeti hii imetenga shilingi Billioni 7, kwa ajili ya
kumalizia miradi yote viporo katika Kata zetu. Tunaamini kwa Bajeti hii itaenda
kujibu na kumaliza matatizo yote, hilo ni jambo la kujivunia sana” alisema Mng’ong’o.
Aidha, Diwani, Wendo Kutusha, alipongeza
Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kufanya kazi kubwa katika kata kwa kutoa
fedha kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. “Kutengewa shilingi Milioni 150 kwa
kila kata kwa ajili ya miradi ya maendeleo, sisi madiwani tunashukuru na
tutahakikisha zinatumika kwa usahihi. Dodoma yetu itabadilika na litakuwa Jiji
la mfano” alisema Kutusha.
MWISHO
Comments
Post a Comment