Baraza la Madiwani la Jiji la Dodoma lapitisha Hesabu za Mwaka 2023/2024
Na. Valeria Adam, DODOMA
Baraza la Madiwani la Jiji la Dodoma limefunga rasmi hesabu za mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni 2024, baada ya kupokea, kujadili na kupitisha taarifa ya ufungaji wa hesabu za halmashauri.
Kwa mujibu wa Mweka Hazina wa Halmashauri ya
Jiji, CPA. David Rubibira alisema chanzo kikuu cha mapato ya halmashauri hiyo
ni tozo, faini na ushuru mbalimbali. Mapato mengine yanatokana na michango ya
afya, uwekezaji, pamoja na ruzuku kutoka Serikali Kuu, aliongeza.
"Mapato na matumizi ya ndani ya
halmashauri ni pamoja na mapato yenye tozo (kodi) ambayo ni kiasi cha shilingi
bilioni 34.7, faini na tozo ni shilingi bilioni 2.6, Mapato mengineyo ni shilingi
bilioni 6.6. Michango mengineyo ya afya ni shilingi bilioni 1.9, mapato
yapatikanayo kwenye uwekezaji ni shilingi bilioni 5.5 na mapato toka serikali
kuu ni shilingi bilioni 83.08 ambapo jumla ya mapato na matumizi yote ya ndani
ya halmashauri ni shilingi bilioni 134.4" alisema CPA. Rubibira.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya
Chang'ombe, Bakari Fundikira alisisitiza kuwa taarifa hiyo ni muhimu katika
kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa shughuli za halmashauri kwa mwaka ujao wa
fedha.
Alibainisha kwamba, kuweka mambo sawa katika
shughuli za halmashauri itawasaidia kujiandaa vyema kwa ajili ya ukaguzi wa
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Fundikira alieleza kuwa baraza linapaswa
kuhakikisha kuwa hakuna mapungufu yanayoweza kuathiri tathmini ya utendaji wa
halmashauri.
"Taarifa hii itupe dira ya utekelezaji
wa shughuli zetu zote za halmashauri katika kuhakikisha tunaweka mambo sawa.
Hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali atakapokuja, basi mambo
mengine tuwe tumeyaweka sawa tayari," alisema Fundikira akihitimisha
mchango wake kwenye mkutano huo.
MWISHO
Comments
Post a Comment