Mstahiki Meya Jiji la Dodoma ahimiza Uwajibikaji

Na. Francisca Mselemo, DODOMA

Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri kupokea na kujadili taarifa ya kufunga hesabu hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2024.

Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, CPA David Rubibira


Akiwasilisha taarifa hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, CPA David Rubibira alisema kuwa taarifa hiyo inawasilishwa kwa mujibu wa sheria. “Mheshimiwa Mstahiki Meya, hesabu hizi sio ngeni. Naomba Baraza lako tukufu lifahamu kwamba ni zilezile ambazo huwa tunakutana na kuzijadili kila robo, za mapato na matumizi. Hii ni kwamba tu ni takwa la kisheria. Tunatakiwa tuziandae katika mpango wa uwasilishaji wa kimataifa. Umuhimu wa hizi hesabu ni kwamba ni takwa la kisheria, kwa maana tunapomaliza mwaka, kwa Halmashauri tunatakiwa kuwa na hesabu za mwaka husika, ambazo katika kipindi kisichozidi miezi mitatu baada ya mwaka kuisha, zinatakiwa ziwasilishwe kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali” alisema CPA Rubibira.

Awali akifungua mkutano huo, Mwenyekiti Prof. Davis Mwamfupe alitoa taarifa kuhusu mabadiliko kadhaa yaliyoamuliwa kufanyika kwa lengo la kuboresha ufanisi wa vikao na kusisitiza muda wa kuanza vikao hivyo na uwajibikaji. “Tumekubaliana na Mkurugenzi kufanya mabadiliko juu ya namna ya uendeshaji wa vikao. Lengo ni kuongeza ufanisi, vikao vianze kwa wakati, vitumie muda mfupi, watu waondoke, waende wakafanye shughuli nyingine za ujenzi wa taifa. Lakini kubwa ninalolisisitiza, tuongeze uwajibikaji katika utendaji wetu wa kazi. Wananchi waone sababu ya uwepo wetu katika nafasi hizi” alisema Prof. Mwamfupe.



Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani ulikuwa na ajenda moja ya kuwasilisha taarifa ya kufunga hesabu za za halmashauri kuishia tarehe 30 Juni 2024, ukihudhuriwa na madiwani, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakuu wa divisheni na vitengo na wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Dodoma pamoja na wakuu wa taasisi za serikali.

MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma