Madiwani Jiji la Dodoma wapitisha taarifa ya ufungaji hesabu za mwaka 2023/2024
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma
limepokea taarifa ya ufungaji wa hesabu kuishia tarehe 30 Juni, 2024 na
kushauri kuwa changamoto zilizojitokeza katika mwaka ulioisha zitatuliwe ili
zisijitokeze katika ufungaji hesabu ujao.
Mwenyekiti wa Mkutano huo, Prof. Davis Mwamfupe akifungua mkutano |
Baada ya taarifa ya ufungaji wa hesabu kuishia tarehe
30/6/2024 kuwasilishwa kwenye mkutano maalum wa Baraza la Madiwani kwa ajili ya
kupitia na kujadili taarifa ya ufungaji wa hesabu iliyowasilishwa na Mkuu wa
Kitengo cha Uhasibu na Fedha Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wajumbe waliipokea.
Mwenyekiti wa Mkutano huo, Prof. Davis Mwamfupe
aliwahoji wajumbe kama wanaipokea taarifa hiyo na kwa kauli moja waliipokea
taarifa hiyo. Alisema kuwa taarifa hiyo imehusisha mapendekezo ya Kamati ya
Fedha na Utawala kama walivyoshauri.
Akiwasilisha taarifa ya ufungaji hesabu za halmashauri
kuishia tarehe 30 Juni, 2024, Mkuu wa Kitengo cha Fedha na Uhasibu, CPA David Rubibira
alisema kuwa taarifa hiyo inatokana taarifa za fedha ambazo huwasilishwa kwenye
vikao vya kamati ya fedha na utawala kila mwezi.
CPA. David Rubibira akiwasilisha taarifa |
Akiongelea umuhimu wa kuwasilisha taarifa hizo,
alisema kuwa ni takwa la kisheria kuandaa hesabu kwa mfumo wa kimataifa yaani ‘International Public Sector Accounting
Standard’ (IPSAS). “Umuhimu ni takwa la kisheria kwamba unapomaliza mwaka wa
fedha halmashauri inatakiwa kuwa na hesabu za mwaka husika zilizowasilishwa kwa
Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ndani ya kipindi cha miezi 3.
Kwa mujibu wa Kanuni ya Fedha ya Serikali za Mitaa ya mwaka 2009, kifungu cha
31 na kifungu namba 45 cha Sheria ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 na marejeo
yake ya mwaka 2000 kinatutaka kuandaa hizo hesabu na kuziwasilisha. Hivyo,
baraza lako lazima lizipitie na kutoa maoni kwenye hizo hesabu ili
tuziwasilishe kwa wakati” alisema CPA Rubibira.
Akiongelea maudhui ya taarifa hiyo, alisema kuwa
inahusisha taarifa ya mali na madeni, mizania ya fedha, mapato na matumizi na
mtiririko wa fedha. Maeneo mengine aliyataja kuwa ni utendaji kazi wa
menejimenti kwa kushirikiana na madiwani, uhai wa halmashauri, taarifa hiyo
inaonesha pia akaunti za halmashauri hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2024, pamoja
na mambo mengine.
Diwani wa Kata ya Chang’ombe, Bakari Fundikira akichangia taarifa ya ufungaji hesabu za halmashauri |
Akichangia taarifa hiyo, Diwani wa Kata ya Chang’ombe,
Bakari Fundikira alisema kuwa taarifa hiyo ni dira kwa mwaka wa fedha
unaoendelea. “Tumeipokea taarifa na kuipongeza timu ya wataalam kwa uandaaji
mzuri wa taarifa. Taarifa imetupa dira ya mwaka huu wa fedha ambao tunao. Yale
mapungufu tukayafanyie kazi ili taarifa ya mwaka huu iwe bora zaidi na madeni
yaweze kupungua kwa kiasi kikubwa. Taarifa hii itupe dira ya utekelezaji wa
shughuli za halmashauri” alisema Fundikira.
MWISHO
Comments
Post a Comment