Hospitali ya Wilaya ya Dodoma kusogeza huduma kwa wananchi

Na. Dennis Gondwe, NALA

Halmashauri ilianza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Dodoma kwa lengo la kusogeza huduma za afya kwa wananchi ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dkt. Revocatus Baltazary alipokuwa akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Dodoma mbele ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma.


Dkt. Baltazary alisema “kutokana na changamoto ya kukosa hospitali ya wilaya kwa muda mrefu na changamoto ya umbali wa kupata huduma za afya kwa ngazi ya wilaya, halmashauri na serikali kuu iliamua kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Dodoma ili kusogeza huduma kwa wananchi. Hatua hii itawezesha wananchi kupata huduma za afya kwa ngazi ya wilaya”.


Akiongelea mapokezi ya fedha, alisema kuwa serikali kuu ilitoa kiasi cha shilingi 1,500,000,000 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. “Awamu ya kwanza halmashauri ilipokea kiasi cha shilingi 1,000,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya maabara, wagonjwa wa nje, mama na mtoto na kichomea taka. Awamu ya pili halmashauri imepokea kiasi cha shilingi 500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la dawa, mionzi na jengo la kuhifadhia maiti. Hadi hatua iliyofikia, jumla ya shilingi 1,477,344,488 zimetumika na hivyo, kubakia na salio la shilingi 22,655,512” alisema Dkt. Baltazary.


Alisema kuwa mradi huo unatekelezwa kwa muda wa miezi sita kwa utaratibu wa “Force Account” ukisimamiwa na kamati tatu za ujenzi, manunuzi na mapokezi unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Julai, 2024.


Baada ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa, Donald Mejiti alisema kuwa mradi huo ni mzuri na unaakisi uhalisia na matumizi sahihi ya fedha. Alisema kuwa hospitali hiyo imejengwa eneo la kimkakati kwa sababu eneo la Nala ni kitovu cha viwanda katika jiji hilo.


Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni moja kati ya halmashauri nane za Mkoa wa Dodoma, ina jumla ya Vituo 45 vya kutolea huduma, kati hivyo, vituo 38 ni zahanati na sita ni vituo vya afya. Idadi kubwa ya wananchi wanapata huduma za afya ngazi ya wilaya katika Hospitali ya Mtakatifu Gemma iliyopo Kata ya Miyuji.

 

MWISHO

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma