CCM yawapongeza walimu Zuzu Sec
Na. Dennis Gondwe, ZUZU
KAMATI ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa
wa Dodoma imewashukuru walimu wa Shule ya Sekondari Zuzu kwa kazi ya
ufundishaji na kusimamia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu shuleni hapo.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa, Donald Mejiti akisisitiza jambo
Shukrani hizo zilitolewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha
Mapinduzi Taifa, Donald Mejiti alipoongoza Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dodoma
kutembelea na kukagua ujenzi wa vyumba nane na matundu 10 ya vyo Shule ya Sekondari
Zuzu.
Mejiti alisema “nianze kwa kutoa pongezi kwa kazi
nzuri mliyofanya na inaonekana. Walimu wetu tunawashukuru sana kwa kazi ya
kufundisha wanafunzi na kusimamia ujenzi wa miundombinu katika shule hii. Nia ya
mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kujenga majengo haya ni kuwawezesha
watoto wetu wasome katika mazingira bora na salama. Watoto wetu wakisoma fursa
za ajira zinakuwa nyingi. Lakini pia amejenga vyuo vya VETA ili kuongeza wigo
kwa watoto wetu, bahati nzuri VETA ada yake ni nafuu sana”.
Aidha, alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji
la Dodoma kwa kuchimba kisima cha maji katika shule hiyo. “Mkurugenzi wa Jiji
ametafsiri maono ya mheshimiwa rais ya kuboresha mazingira ya kufundishia na
kujifunzia kuwa bora kwa kuchimba kisima cha maji shuleni hapa. Wote tunafamahu
umuhimu wa maji katika taasisi kama hii” alisema Mejiti.
Awali akimkaribisha Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM
Taifa, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alisema kuwa kazi nzuri
imefanyika Shule ya Sekondari Zuzu katika ujenzi wa miundombinu na utunzaji wa
mazingira. “Mgeni rasmi shule hii ipo mstari wa mbele katika kupanda miti na
kutunza mazingira. Nimpongeza sana Mkurugenzi wa Jiji kwa kutoa shilingi
milioni 20 kuchimba kisima cha maji hapa. Pia shilingi milioni 85 zimetolewa
kwa ajili ya kukamilisha maabara” alisema Alhaj Shekimweri.
Akisoma taarifa ya
ujenzi wa vyumba nane vya madarasa na matundu 10 ya vyoo kwa Kamati ya Siasa ya
CCM Mkoa wa Dodoma Mkuu wa Shule ya Sekondari Zuzu, Mwl Herzon Emmanuel alisema
kuwa shule hiyo katika miaka mitano iliyopita haikuwa na ufaulu mzuri, baada ya
uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya awamu ya sita imepelekea ufaulu wa
shule kuongezeka na hamasa ya wanafunzi kujiunga na shule imeongezeka sana. Alisema
kuwa kwa matokeo ya kidato cha Nne 2023 shule imepata mwanafunzi wa kwanza
aliyefaulu kwa daraja la kwanza tangu shule ianzishwe.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Zuzu, Mwl Herzon Emmanuel akisoma taarifa ya mradi
Kuhusu mapokezi ya fedha
alisema kuwa shule ilipokea jumla ya shilingi 201,000,000.00 kutoka serikali kuu
kwa ajili ya ujenzi wa vyumba nane vya madarasa na matundu 10 ya vyoo. Fedha hiyo
iliingia katika akaunti ya shule tarehe 05/01/2024.
Akiongelea umuhimu wa shule hiyo Katibu Kata wa
CCM Kata ya Zuzu, Suma Kyomola alisema kuwa shule hiyo imekuwa suluhu kwa watoto
wa kata hiyo. “Baadhi ya watoto waliosoma shuleni hapa wameshanufaika na ajira
mbalimbali wengine wapo vyuoni, wengine kwenye taasisi za dini na wengine
kwenye sekta ya afya” alisema Kyomola.
Shule ya Sekondari Zuzu
ni shule ya serikali iliyoanzishwa mwaka 2007, imekuwa chachu kubwa ya utoaji
wa elimu katika Kata ya Zuzu ikiwa umbali wa Kilometa 14 kutoka katikati ya Jiji
la Dodoma ikiwa na jumla ya wanafunzi 442.
MWISHO
Comments
Post a Comment