Kituo cha Afya Ilazo kuboresha huduma ya mama na mtoto
Na. Dennis Gondwe, NZUGUNI
MRADI wa ujenzi wa Kituo
cha Afya Ilazo utawezesha kutoa huduma za upasuaji, kliniki ya mama na mtoto na
huduma za kujifungua zikiwa zimeunganishwa na mfumo wa hewa ya Oksijeni.
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu
Mganga Mkuu wa Jiji la Dodoma, Dkt. Revocatus Baltazary alipokuwa akisoma
taarifa ya mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Ilazo kwa Kamati ya Siasa ya Mkoa
wa Dodoma ilipotembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Jiji
la Dodoma.
Dkt. Baltazary alisema “mradi
huu utawezesha kutoa huduma za
upasuaji, kliniki
ya mama na mtoto, huduma za kujifungua, wodi ya watoto wachanga, huduma
za kuhifadhi miili. Wodi
hizi pia zimeunganishwa na mifumo ya hewa ya Oksijeni ambayo ipo
katika wodi ya wazazi, watoto na jengo la upasuaji. Mifumo hii itasaidia
wagonjwa wote wenye changamoto ya upumuaji kupata huduma hapa kituoni. Aidha, huduma za lishe zitatolewa ikiwemo
elimu juu ya masuala ya lishe, upimaji wa hali za lishe na ushauri”.
Akiongelea lengo na gharama za mradi huo alisema
ni kuboresha huduma za mama na mtoto na huduma za upasuaji. “Gharama ya mradi
huu hadi utakapokamilika ni shilingi 3,094,983,663.32
kati ya fedha hizo shilingi 2,870,483,663.32 ni gharama za ujenzi na shilingi
224,500,000.00 ni kwa ajili ya mshauri mwelekezi na hadi hatua hii iliyofikia
kiasi cha shilingi 2,583,435,296.98 kimetumika. Kwa sasa Jiji la Dodoma
limepokea baadhi ya vifaa tiba vitakavyotumika katika mradi huu kutoka Shirika
la kimataifa la kuhudumia watoto (UNICEF). Pia watumishi 17 watakaotoa huduma
katika kituo hiki wameshajengewa uwezo na kwa hivi sasa wako katika vituo
mbalimbali wakiendelea kuongeza uzoefu” alisema Dkt. Baltazary.
Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Ilazo unajengwa chini ya ufadhili wa KOICA
kupitia Shirika la kimataifa la kuhudumia watoto UNICEF, ukiwa unatekelezwa
katika Kata ya Nzunguni, Mtaa wa Ilazo ukitarajiwa kuhudumia wananchi zaidi ya 99,743.
MWISHO
Comments
Post a Comment