Sekondari Zuzu yapongezwa na CCM Mkoa
Na. Dennis Gondwe, ZUZU
KAMATI ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma imewashukuru walimu wa Shule ya Sekondari Zuzu kwa kazi ya ufundishaji na kusimamia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu shuleni hapo.
Shukrani hizo zilitolewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa, Donald Mejiti alipoongoza Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dodoma kutembelea na kukagua ujenzi wa vyumba nane na matundu 10 ya vyo Shule ya Sekondari Zuzu.
Mejiti alisema “nianze kwa kutoa pongezi kwa kazi nzuri mliyofanya na inaonekana. Walimu wetu tunawashukuru sana kwa kazi ya kufundisha wanafunzi na kusimamia ujenzi wa miundombinu katika shule hii. Nia ya mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kujenga majengo haya ni kuwawezesha watoto wetu wasome katika mazingira bora na salama. Watoto wetu wakisoma fursa za ajira zinakuwa nyingi. Lakini pia amejenga vyuo vya VETA ili kuongeza wigo kwa watoto wetu, bahati nzuri VETA ada yake ni nafuu sana”.
Aidha, alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuchimba kisima cha maji katika shule hiyo. “Mkurugenzi wa Jiji ametafsiri maono ya mheshimiwa rais ya kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kuwa bora kwa kuchimba kisima cha maji shuleni hapa. Wote tunafamahu umuhimu wa maji katika taasisi kama hii” alisema Mejiti.
Awali akimkaribisha Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alisema kuwa kazi nzuri imefanyika Shule ya Sekondari Zuzu katika ujenzi wa miundombinu na utunzaji wa mazingira. “Mgeni rasmi shule hii ipo mstari wa mbele katika kupanda miti na kutunza mazingira. Nimpongeza sana Mkurugenzi wa Jiji kwa kutoa shilingi milioni 20 kuchimba kisima cha maji hapa. Pia shilingi milioni 85 zimetolewa kwa ajili ya kukamilisha maabara” alisema Alhaj Shekimweri.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa vyumba nane vya madarasa na matundu 10 ya vyoo kwa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dodoma Mkuu wa Shule ya Sekondari Zuzu, Mwl Herzon Emmanuel alisema kuwa shule hiyo katika miaka mitano iliyopita haikuwa na ufaulu mzuri, baada ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya awamu ya sita imepelekea ufaulu wa shule kuongezeka na hamasa ya wanafunzi kujiunga na shule imeongezeka sana. Alisema kuwa kwa matokeo ya kidato cha Nne 2023 shule imepata mwanafunzi wa kwanza aliyefaulu kwa daraja la kwanza tangu shule ianzishwe.
Kuhusu mapokezi ya fedha alisema kuwa shule ilipokea jumla ya shilingi 201,000,000.00 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa vyumba nane vya madarasa na matundu 10 ya vyoo. Fedha hiyo iliingia katika akaunti ya shule tarehe 05/01/2024.
Akiongelea umuhimu wa shule hiyo Katibu Kata wa CCM Kata ya Zuzu, Suma Kyomola alisema kuwa shule hiyo imekuwa suluhu kwa watoto wa kata hiyo. “Baadhi ya watoto waliosoma shuleni hapa wameshanufaika na ajira mbalimbali wengine wapo vyuoni, wengine kwenye taasisi za dini na wengine kwenye sekta ya afya” alisema Kyomola.
Shule ya Sekondari Zuzu ni shule ya serikali iliyoanzishwa mwaka 2007, imekuwa chachu kubwa ya utoaji wa elimu katika Kata ya Zuzu ikiwa umbali wa Kilometa 14 kutoka katikati ya Jiji la Dodoma ikiwa na jumla ya wanafunzi 442.
MWISHO
Comments
Post a Comment