Ukarabati Shule ya Msingi Iyumbu kupunguza msongamano darasani
Na. Dennis Gondwe, IYUMBU
MRADI wa ukarabati wa
vyumba 10 vya madarasa katika Shule ya Msingi Iyumbu umesaidia kupunguza
msongamano wa wanafunzi darasani na kuwaboreshea wanafunzi mazingira bora ya
kujifunzia.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Iyumbu, Mwl. Monica Nshimba
Kauli hiyo ilitolewa na Mwalimu
Mkuu wa Shule ya Msingi Iyumbu, Mwl. Monica Nshimba alipokuwa akisoma taarifa
ya mradi wa ukarabati wa vyumba 10 vya madarasa katika Shule ya Msingi Iyumbu
kwa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma ilipotembelea
shule hiyo iliyopo Kata ya Iyumbu jijini Dodoma.
Mwl. Nshimba alisema “ukarabati
wa mradi umepunguza kwa kiasi
kikubwa msongamano wa wanafunzi darasani kwasababu kabla ya ukarabati, kulikuwa
na vyumba vinne ambavyo vilikuwa havitumiki kabisa na hata vile vilivyokuwa
vinatumika vilikuwa katika hali mbaya sana. Hivyo, kwa sasa vyumba vyote vinatumika.
Pia mazingira ya kujifunzia na kufundishia yamekuwa mazuri na rafiki kiasi
kwamba wanafunzi na walimu wote tunayafurahia. Hivyo, kuongeza ari ya kufanya
kazi na kujifunza”.
Akiongelea mapokezi ya fedha, alisema kuwa shule yake
ilipokea fedha kiasi cha shilingi 90,000,000.00
kutoka Serikali Kuu tarehe 05 Januari, 2024 kwa ajili ya ukarabati wa vyumba 10
vya madarasa. “Mradi huu ulianza kutekelezwa tarehe 15 Januari, 2024 na
umetekelezwa kwa kutumia ‘Force Account’ ambapo kulikuwa na kamati tatu za Ujenzi,
Manunuzi na Kamati ya Mapokezi na Ukaguzi. Kamati hizi zilikuwa na uwakilishi
wa wananchi wa Kata ya Iyumbu ambao wameshiriki katika usimamizi wa mradi hadi
kukamilika. Mradi umetumia jumla ya shilingi 90,000,000.00 ambapo imejumuisha malipo
ya wazabuni, fundi na kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Mradi
umekamilika kwa asilimia 100 uliohusisha ukarabati wa vyumba 10 vya madarasa na
ofisi mbili umekamilika tarehe 30 Aprili, 2024 na mradi unatumika” alisema Mwl.
Nshimba.
Ikumbukwe kuwa Shule ya Msingi Iyumbu ilianzishwa
mwaka 1980 sasa ina wanafunzi 1,219 kati yao wavulana ni 561 na wasichana ni 658
ikijivunia kufanya vizuri kitaaluma kwa kuongeza ufaulu kwa darasa la Saba kwa
miaka mitatu mfululizo.
MWISHO
Comments
Post a Comment