Waziri Mavunde asisitiza miradi mikubwa ya madini iliyopewa leseni kuanza kazi haraka
Na. Mwandishi Wetu, DODOMA
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde,
ameagiza miradi mikubwa na ya kati ya Madini ambayo tayari imekwishapewa leseni
kuanza utekelezaji wake mara moja ili kuchochea ukuaji wa sekta na kuleta
manufaa kwa taifa na kutimiza azma ya serikali kutoa leseni hizo.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde |
Aliyasema jijini Dodoma wakati akizungumza katika mkutano maalum na Chemba ya Migodi Tanzania (TCM) kwa lengo kujadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya Madini ili kuboresha uendelezaji na usimamizi wa shughuli za uchimbaji na biashara ya Madini kwa manufaa ya sekta na taifa kwa ujumla.
Waziri Mavunde alisema serikali inataka
kuhakikisha kuwa miradi yote ya uchimbaji Madini iliyopangwa kuanza inaanza
mara moja bila kucheleweshwa, na kuwa serikali kwa upande wake imejitahidi
kurahisisha taratibu kwa wawekezaji na sasa ni wakati wa sekta binafsi kuchukua
hatua kwa upande wao.
“Serikali imefanya kazi yake, tumeondoa
vikwazo vingi na kurahisisha utaratibu. Sasa ni jukumu la wawekezaji
kuhakikisha kuwa miradi inaanza kutekelezwa mara moja” alisema Waziri Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde aliahidi kuwa
Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa madini, ikiwemo TCM, katika
kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji ili kuhakikisha sekta hiyo
inaendelea kukua kwa kasi na kufikia lengo la uchangiaji wake katika Pato la
Taifa (GDP) na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla.
“Sisi kama serikali tutakaa pamoja na taasisi husika ili kuangalia changamoto zilizopo na kuzitatua kwa haraka. Hatutaki ukiritimba wowote ambao unaweza kuchelewesha maendeleo ya sekta hii muhimu, serikali hii ni moja na ina lengo moja” alisisitiza Mavunde.
Kwa upande mwingine, Waziri Mavunde alisisitiza
umuhimu wa utafiti katika sekta ya Madini, akieleza kuwa maendeleo endelevu
yanategemea uwekezaji mkubwa katika tafiti zinazosaidia kuongeza uzalishaji na
tija. Aidha, amepongeza juhudi za wadau wa sekta hiyo katika kutekeleza Maono
ya Vision 2030; Madini ni Maisha na Utajiri inayotekelezwa na Wizara kwa lengo
la kuongeza maeneo yaliyofanyiwa utafiti wa kina, kuongeza ajira kwa
Watanzania, Miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR), na uwezeshaji wa
Watanzania kupitia Ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content).
Kuhusu mchango wa Sekta ya Madini kwenye
uchumi wa taifa, Waziri Mavunde ameeleza kuwa Sekta hiyo imeendelea kukua kwa
kasi, ambapo mwaka 2022/23 ilichangia asilimia 7.2 ya Pato la Taifa, huku mwaka
2023/24 mchango wake ukifikia asilimia 9.0. Serikali inalenga Sekta hiyo
ichangie angalau asilimia 10 ifikapo mwaka 2025, kama ilivyoainishwa kwenye
Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 pamoja na
Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2025.
Katika ukusanyaji wa Maduhuli ya
Serikali, Waziri Mavunde amesema mapato yameongezeka maradufu, ambapo mwaka wa
fedha wa 2015/16 yalikuwa shilingi bilioni 162, lakini kufikia mwaka wa fedha
2023/24 yaliongezeka hadi shilingi bilioni 753 ambapo kwa mwaka huu wa fedha wa
2024/25, Serikali inalenga kukusanya shilingi trilioni 1, lengo ambalo
linaonekana litafikiwa kulingana na mwenendo wa ukusanyaji mapato.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Chemba ya
Migodi Tanzania (TCM) Mhandisi Benjamin Mchwampaka aliipongeza serikali kupitia
Wizara ya Madini kwa kuendelea kuwashirikisha katika hatua mbalimbali za
majadiliano kwa lengo la kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji nchini.
Alisema kuwa, Tanzania ni moja ya nchi
chache ambazo sekta binafsi inapewa nafasi ya kushiriki vikao muhimu sambamba
na Maafisa wa Serikali akitolea mfano ushiriki wa pamoja wa Wizara na TCM
katika mikutano mikubwa kama Mining Indaba ambayo hufanya Afrika Kusini kila
mwaka.
Chanzo: Fullshangwe Blog
Comments
Post a Comment