Nyumba ya mtumishi kuchangia huduma masaa 24 Zahanati ya Ipala
Na. Nancy Kivuyo, IPALA
Mradi
wa ujenzi wa nyumba ya mtumishi katika Zahanati ya Ipala uliogharimu kiasi cha shilingi
55,000,000, umeleta maboresho katika utoaji wa huduma ya afya katika kata hiyo.
Nyumba ya Mtumishi Zahanati ya Ipala |
Hayo
yalielezwa na Muuguzi kutoka Zahanati ya Ipala, Tumain Sanga alipokuwa
akiwaelezea waandishi wa habari waliofanya ‘media tour’ kutembelea miradi ya
maendeleo iliyotekelezwa na serikali katika kata hiyo kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.
Alisema
kuwa anatoa pongezi kwa serikali kuwajengea nyumba hiyo ili kurahisisha utoaji
wa huduma za afya katika kata hiyo. “Tunaipongeza serikali kutujengea nyumba ya
mtumishi, uwepo wa nyumba hii imeturahisishia kutendaji wa kazi mzuri. Laiti
tungekuwa mbali tungeshindwa kuwahudumia wananchi vizuri na kwa wakati, lakini
sasa wagonjwa wanaweza kuja muda wowote na wakatukuta na tukawahudumia kwa masaa
24. Tunaishukuru sana serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa
na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunamshukuru Mbunge wetu Anthony Mavunde na
Diwani George Magawa kwa kutusemea huko kwenye vikao na mapendekezo mengine
mpaka wakaona Kata ya Ipala inastahili kujengewa nyumba ya mtumishi ili
kusogeza huduma karibu kwa wananchi” alisema Sanga.
Tumain Sanga, Afisa Muuguzi Zahanati ya Ipala |
Nae
Diwani wa Kata ya Ipala, George Magawa aliongeza kwa kusema, Jiji la Dodoma ni
kubwa sana kuna kata nyingine hazijapata kipaumbele hicho, hivyo anaipongeza
serikali kwa juhudi hizo za kuwasogezea huduma ya afya wakazi wa Ipala ambapo
kiasi cha 55,000,000 kimetolewa na serikali kuu, ujenzi umekamilika na nyumba
inatumika . “Awali ya yote tumefanya ukarabati wa zahanati ambayo ilikua
imechakaa, pili tukaona ni vyema kujenga nyumba ya mganga katika eneo la
zahanati ili kusogeza huduma kwa masaa 24 ili wakati wowote mganga anahitajika
kutoa huduma apatikane kwa urahisi” alimalizia Magawa.
Kwa upande mwingine, mkazi wa Kata ya Ipala, David Mhuna aliishukuru serikali kwa kukarabati zahanati pamoja na kujenga nyumba ya mganga. “Ni jambo jema hapa kwenye kata yetu kuwa na makazi ya watumishi karibu na zahanati. Huduma imesogea karibu hivyo hata ikitokea usiku mtu amepata dharura itakuwa rahisi kuhudumiwa kwa wakati. Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita kwa kutujali” alishukuru Mhuna.
MWISHO
Comments
Post a Comment