Shule shikizi Ipala, mkombozi kwa wanafunzi wanaotembea umbali mrefu
Na. John Masanja, IPALA
Diwani
wa Kata ya Ipala, George Magawa, aishukuru serikali ya awamu ya sita
inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu ya
elimu msingi katika kata hiyo kwa kujenga shule shikizi ili kutengeneza
mazingira rafiki kwa wanafunzi wenye umri mdogo kupata elimu bora.
Diwani wa Kata ya Ipala, George Magawa |
Aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari waliofanya ‘media tour’ kutembelea miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali katika Kata ya Ipala kuanzia mwaka 2021 hadi 2025.
Diwani
Magawa alisema kuwa katika miaka minne ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita,
elimu katika Kata ya Ipala imekuwa kwa kasi. “Serikali yetu tukufu imetuletea
elimu hadi kwenye kata yetu. Tuna shule shiziki mbili zimeanzishwa kwa lengo la
kusaidia wanafunzi wadogo wanaotembea umbali mrefu karibu kilomita tano kufuata
elimu. Sasa hivi uwepo wa madarasa haya matatu nafuu imekuwa kubwa sana kwa
kuwapunguzia watoto wadogo kutembea umbari mrefu” alisema Magawa.
Pia,
aliongeza kuwa anaishukuru serikali kwa maboresho hayo kwasababu wanafunzi
wanapata elimu ipasavyo na anaamini kwa siku zijazo maboresho makubwa zaidi
yatafanyika. “Tunaishukuru serikali kuanzia rais wetu Dkt. Samia, Mbunge
Mavunde, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Dkt. Sagamiko na watendaji wengine wote
kwa kuona umuhimu mkubwa wa Kata ya Ipala kupata shule hizi. Kama mlivyojionea
ndugu waandishi, jiji hili ni kubwa kwahiyo, hata sasa tunafurahi kufikiwa na
maendeleo haya” alishukuru Magawa.
Kwa
upande mwingine, mkazi wa Kata ya Ipala, Elisha Nghambi alimshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada nyingi
anazofanya kuboresha maendeleo ya wananchi ikiwemo sekta ya elimu. “Shule hii
shikizi ya Mwinyi imekuwa na faida kubwa hasa kwa kuinua viwango vya elimu hapa
kwetu, hapo nyuma vijana wengi hawakusoma kutokana na umbali uliokuwepo. Ujenzi
wa shule hii umeleta mwamko wa elimu zaidi, wazazi wanapeleka watoto shule, watoto
wengi wa mtaa huu wanasoma na kufurahia sasa, tunashukuru sana. Mradi huu ni
chachu ya wananchi kuwahimiza watoto kupata elimu ili kutenegeneza maisha yao
ya sasa na ya baadae” alishukuru Nghambi.
MWISHO
Comments
Post a Comment