Jiji la Dodoma kuanza ujenzi wa Jengo Jumuishi Kituo cha Afya Makole

Na. Faraja Mbise, MAKOLE

Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatarajia kuanza ujenzi wa Jengo Jumuishi katika Kituo cha Afya Makole ambao unatarajiwa kuanza tarehe 27 Januari, 2025 chini ya Mkandarasi Mohanmmedi Builders Limited.




Akizungumzia kuhusu huduma zitakazokuwa zinapatikana katika jengo hilo jumuishi Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makole, Dkt. Revocatus Baltazary alisema zitapatikana huduma mbalimbali kwa ajili ya kukidhi huduma zote za kiafya. “Jengo hili linaenda kujibu yote hayo, kwasababu huduma zitakazoenda kupatikana ni huduma za ‘emergency’, radiolojia, maabara, vyumba vya madaktari vitaongezwa. Pia kuna wodi za kulaza watoto chini ya umri wa miaka mitano, magonjwa ya ndani kwa wanawake na wanaume. Vilevile, wodi za upasuaji na ‘floor’ ya wakina mama wajawazito” alisema Dkt. Baltazary.

Sambamba na hilo, alisema kuwa lengo hasa la kujenga jengo hilo ni kukosekana kwa baadhi ya huduma kama ‘emergency’, huduma za kulaza, na jengo la upasua. “Jengo hili linajengwa kutokana na baadhi ya huduma zinazokosekana katika Kituo cha Afya Makole ikiwepo huduma za ‘emergency’, huduma za kulaza, lakini pia ‘theatre’ ipo moja na pia wodi za upasuaji. Kwahiyo, jengo hili linaenda kujibu yote hayo”.

Kwa upande wake Mhandisi wa Jiji, Nicodemus Kileo, alisema kuwa wanatarajia utekelezaji wa mkataba wa ujenzi huo utakamilika ndani ya wakati uliopangwa. Pia alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kutoa fedha ya ujenzi wa vituo vya Afya. “Ni matarajio yetu kwamba, utekelezaji wake utaenda ‘smooth’ na utakamilika ndani ya ule muda uliopangwa na tunategemea usizidi. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa fedha ambazo zimetolewa ikiwa na lengo la kukidhi haja na mahitaji ya mji inayopelekea kuwa na changamoto kubwa ya masuala ya kiafya” alisema Mhandisi Kileo.

Nae, Mkandarasi kutoka Mohammedi Builders Limited, Meneja Mohammed Jafferji, alisema kuwa, anategemea kukamilisha ujenzi wa mradi huo kabla ya muda uliopangwa. “Tunategemea kuanza ujenzi kuanzia Jumatatu tarehe 27 Januari, 2025 na itatuchukua mwaka mmoja kukamilisha mradi huo kama ‘contract’ inavyosema. Lakini tutajitahidi kukamilisha na kuumaliza kabla ya wakati uliopangwa” alisema Meneja Jafferji.

Mradi wa ujenzi wa Jengo Jumuishi Kituo cha Afya Makole unasimamiwa na Mkandarasi Mohammedi Builders Limited, ambapo amekabidhiwa eneo siku ya tarehe 24 Januari, 2025. Mkataba huo ulisainiwa tarehe 17 Januari, 2025 na utadumu kwa muda wa miezi kumi na miwili.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Osterbay Dodoma wajitokeza usafi wa mazingira

Usafi wa Mazingira Kipaumbele Kata ya Chamwino

Wananchi wa Kata ya Mtumba wanufaika na Mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri