Wakuu wa Shule Jiji la Dodoma wapewa mafunzo ya mfumo wa NeST
Na. Coletha Charles, DODOMA
Wakuu wa Shule za Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dodoma
wamewezeshwa mafunzo ya ununuzi kwa njia ya mtandao serikalini ‘National
e-Procurement System of Tanzania’ (NeST) yatakayoboresha utendaji kazi na
kuwawezesha kupata mafundi na watoa huduma kupitia mfumo wa manunuzi.
Mafunzo hayo yalitolewa na Kitengo
cha Manunuzi na Ugavi kwa lengo la kuongeza ufanisi na uwazi kwa kufanya
shughuli za ununuzi kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Mwaka 2023 na Kanuni za
Manunuzi za Mwaka 2024, katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Umonga.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Afisa
Elimu Vifaa na Takwimu, Fredrick Mwakisambwe, alifafanua mfumo wa manunuzi kwa
njia ya kielektroniki, ni mfumo ambao unarahisisha mchakato wa manunuzi na
kuleta ufanisi mkubwa katika utendaji kazi.
Alisema kuwa mafunzo hayo ni mahususi kwa wakuu wa shule
wakiambatana na walimu wanaohusika kuratibu na kusimamia fedha ambazo
zinapelekwa katika shule za sekondari kwa kuelekezwa namna sahihi ya kutumia
mfumo mpya wa manunuzi ambao ni NeST’. “Ufanisi kwa mwaka 2025 utakuwa
mkubwa hasa katika manunuzi ya vitu mbalimbali vya shule za sekondari. Kwahiyo,
mfumo huu tumeona jinsi ambavyo ulivyokuwa mzuri na huru, ukilinganisha na
utaratibu wa zamani ambao ulikuwa siyo wa mfumo na ulikuwa unapelekea wakati
mwingine udanganyifu au ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi. Tunatarajia
baada ya mafunzo haya walimu wetu watakuwa na uelewa wa kutosha katika matumizi
ya manunuzi ya vifaa kwa kutumia fedha za serikali” alisema Mwakisambwe.
Nae, Muwezeshaji wa mafunzo hayo, Afisa Manunuzi kutoka
Kitengo cha Manunuzi na Ugavi, Mary Ngailo, alieleza
kuwa mfumo mpya wa manunuzi, ‘NeST,’ utaongeza uwazi na ufanisi katika
michakato ya ununuzi serikalini kwa kupunguza gharama na muda unaotumika katika
taratibu za manunuzi kwa kuleta tija kwa taasisi za umma.
Alisema kuwa mfumo
huu utasaidia taasisi nyingi za umma kuboresha ufanisi wa taratibu za manunuzi
‘NeST’, ambao ni jukwaa la kidijitali na kuwezesha uratibu wa zabuni na
ununuzi kwa kutumia teknolojia ya kisasa. “Sheria imeitaka taasisi husika
kutumia njia ya kielektroniki
kufanya manunuzi. Kwahiyo, mwalimu na mzabuni hawaonani ana kwa ana mwalimu
atatuma mapendekezo yake au mahitaji yake kwenye mfumo na mzabuni atakaye kidhi
vigezo ataomba. Lakini kumekuwa na changamoto ya bei inayoombwa na mzabuni
unakuta ipo juu kuliko bei ambayo inakuwa imekadiliwa kuwa ni bei ya soko, baada
ya kutokea shida kama hiyo inafanyika ‘negotiation,’ na kwa sasa sheria
imekuja kukataza matumizi ya kufanya ‘negotiation’ kwa kutumia simu na
badala yake inataka majadiliano yafanywe na timu ya majadiliano ambayo
itateuliwa na afisa masuhuli wa taasisi husika” alisema Ngailo.
Kwa upande wake,
Mkuu wa Shule ya Sekondari Mbabala, Mwl. Patrick Mayengo, alionesha furaha yake
baada ya wakuu wa shule kupata mafunzo ya mfumo mpya wa manunuzi wa ‘NeST’.
Alisema kuwa mfumo huo utaleta mapinduzi katika ufanisi wa ununuzi na
usimamizi wa rasilimali shuleni.
Alisema kuwa mfumo
wa ‘NeST’ utasaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa walimu kwa
kuhakikisha kuwa vifaa vya shule vinanunuliwa kwa haraka, kwa usahihi na kwa
gharama nafuu. “Mfumo huu utakuwa suluhisho la kudumu, kwasababu unahakikisha
usalama na uwazi katika manunuzi yote. Mfumo huu unatusaidia kutangaza zabuni
ambazo mtu anakutana nazo huko kwenye mfumo siyo mpaka nimtafute ‘physically”
alisema Mwl. Mayengo.
MWISHO
Comments
Post a Comment