Uboreshaji daftari la wapiga kura chini ya dakika 5
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WANANCHI katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameshauriwa
kufika katika vituo vya kuandikishia wapiga kura ili kujiandikisha na kuboresha
taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura mapema kwa sababu zoezi
linafanyika chini ya dakika tano.
Faraja Mbise baada ya kujiandikisha |
Ushauri huo ulitolewa na Faraja Mbise, mkazi wa Mtaa wa Chang’ombe, Kata ya Ihumwa, Halmashauri ya Jiji la Dodoma alipofanya
mahojiano maalum baada ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura
katika Kituo cha Shule ya Msingi Msuguri.
Mbise alisema “wito wangu kwa wananchi ambao bado
hawajafika katika vituo vyao vya kujiandikisha, wafike mapema kwa sababu zaidi
ya siku ya leo zitakuwa zimebaki siku mbili tu. Wajitokeze kwa wingi
kujiandikisha kwa sababu zoezi linaenda vizuri sana na kwa haraka. Ni zoezi
ambalo halichukui hata zaidi ya dakika tano”.
Aidha, akiongelea utendaji wa maafisa uandikishaji,
alisema kuwa wanafanya kazi vizuri. “Maafisa uandikishaji wamejipanga vizuri. Wanatoa
huduma vizuri wanapokea watu vizuri sana wanauliza maswali vizuri na utaratibu
ni mzuri, kuna upishano wa haki kati na wanawake kwa wanaume” alisema Mbise.
Faraja Mbise akiongelea utendaji wa maafisa uandikishaji |
Kuhusu sababu za yeye kuwahi zaidi kituoni, alisema
kuwa ana majukumu mengine ya kikazi. “Katika kituo nilichojiandikisha nilikuwa
mwananchi wa tatu. Niliwahi mapema zaidi kujiandikisha ili kuhofia foleni hapo
baadae ili niwe wa mwanzo kuhudumiwa na kuendelea majukumu mengine ya kazi.
Hivyo, wananchi ambao bado hawajaenda vituoni kufanya hivyo, mapema na kuendelea
na majukumu mengine kwa sababu muda wa kuhudumiwa ni mfupi sana” alisisitiza Mbise.
Leo ni siku ya tano tangu kuanza kwa zoezi la
uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma
ukihusisha usajili wa wapiga kura wapya waliotimiza umri wa miaka 18,
kurekebisha, kubadili taarifa au kuhama kituo chini ya kaulimbiu “Kujiandikisha, Kuwa Mpiga Kura ni Msingi
wa Uchaguzi Bora”
MWISHO
Comments
Post a Comment