Vijana wahamasishwa kujiandikisha Daftari la Kudumu la Wapiga kura
Na. Dennis Gondwe, DODOMA MAKULU
VIJANA wameshauriwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha
katika daftari la kudumu la wapiga kura katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili
waweze kushiriki zoezi la Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Magdalena Samwel, mkazi wa Mtaa wa Mwangaza Kata ya Dodoma Makulu
Ushauri huo ulitolewa na Magdalena Samwel, mkazi wa Mtaa
wa Mwangaza Kata ya Dodoma Makulu, Halmashauri ya Jiji la Dodoma muda mfupi
baada ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kwenye kituo
kilichopo Shule ya Sekondari Kisasa leo asubuhi.
Samwel alisema “leo nimewahi hapa kituoni kwa ajili ya
kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ili niwahi kazini. Nimejiandikisha
nikiwa mtu wa pili, ulinitangulia wewe ndugu mwandishi. Nimekuja ili nipate uhalali
kwa kushiriki uchanguzi mkuu ujao kama mtanzania”.
Aidha, alitoa wito kwa vijana kujitokeza kwa wingi
kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura. “Napenda kuwashauri
vijana wajitokeze kwa wingi ili waje kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili
wapata kitambulisho kitakachowasaidia katika kushiriki uchanguzi mkuu ujao”
alisema Samwel.
Wakati huohuo, Halima Shaban, mkazi wa Mtaa wa
Mwangaza, Kata ya Dodoma Makulu baada ya kujiandikisha akiwa mtu wa tatu alisema
kuwa zoezi hilo litawawezesha kushiriki katika kuwachagua viongozi ambao ni Rais,
Wabunge na Madiwani. “Nimekuja kujiandikisha hapa ili nipate kitambulisho
ambacho kitaniwezesha kushiriki uchaguzi na kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani.
Hivyo, niwashauri vijana wenzangu ambao bado hawajafika katika vituo kufika na
kujiandikisha” alisema Shaban.
Halima Shaban, mkazi wa Mtaa wa Mwangaza, Kata ya Dodoma Makulu
Leo ni siku ya tano tangu kuanza kwa zoezi la
uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma
ukihusisha usajili wa wapiga kura wapya waliotimiza umri wa miaka 18,
kurekebisha, kubadili taarifa au kuhama kituo chini ya kaulimbiu “Kujiandikisha, Kuwa Mpiga Kura ni Msingi
wa Uchaguzi Bora”.
MWISHO
Comments
Post a Comment