Jiji la Dodoma lakusanya 103% mapato ya ndani 2023/2024
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imefanikiwa kukusanya fedha
za mapato ya ndani shilingi 51,402,342,226 sawa na asilimia 103 ya lengo la
mwaka wa fedha 2023/2024 wakati ikipeleka fedha nyingi kwenye miradi ya
maendeleo.
Katibu wa Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa Mkutano wa Baraza la
Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo wakati wa Mkutano wa Baraza
la Madiwani wa kupokea na kujadili taarifa za utendaji kazi kwa kipindi cha
robo ya nne (Aprili-Juni, 2024) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma.
Kayombo ambae ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma
alisema kuwa bajeti ya mapato ya ndani ya mwaka 2023/2024 ilikuwa shilingi 50,097,458,280.
Fedha iliyokusanywa ni shilingi 51,402,342,226 sawa na asilimia 103. Alisema kati
ya fedha hizo za mapato ya ndani, asilimia 73.4 ilipelekwa kwenye utekelezaji
wa miradi ya maendeleo na asilimia 26.6 ikienda kwenye matumizi mengineyo.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Kayombo alilipongeza Baraza
la Madiwani kwa kutenga na kutoa fedha za fidia. “Mheshimiwa mwenyekiti, nilipongeze
Baraza la Madiwani kwa kutenga na kutoa fedha. Wananchi 357 wamelipwa fidia
ndani ya kipindi cha miezi sita kiasi cha shilingi bilioni 3.2 kati ya shilingi
bilioni 3.4 zilizotengwa. Hatuna upungufu wa kulipa fidia, ni maelekezo ya Chama
Cha Mapindzi ngazi ya wilaya na mkoa” alisema Kayombo kwa kujiamini.
Wakati huohuo, aliutaarifu mkutano huo kuwa
halmashauri imenunua magari mawili kwa ajili ya kusafisha barabara. Alisema kuwa
gari moja lina uwezo wa kufagia barabara kisha mchanga unaofagiliwa ukafyonzwa.
Gari la pili linauwezo wa kudeki barabara kwa presha ya maji. Alisema kuwa magari
hayo yamenunuliwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Ikumbukwe kuwa mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya
Jiji la Dodoma ilikusanya asilimia 80.6 ya mapato ya ndani.
MWISHO
Comments
Post a Comment