Ujenzi wa Kituo Kipya cha Afya Chang'ombe kusaidia wananchi zaidi ya 200 kwa siku
Na. John Masanja, CHANG’OMBE
Wananchi wa Kata ya Chang’ombe
waishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kupunguza kadhia ya upatikanaji wa
huduma za afya kupitia ujenzi wa Kituo kipya cha Afya Chang’ombe.
Diwani wa Kata ya Chang’ombe, Bakari Fundikila akifafanua jambo
Akizungumza katika mahojiano maalum
na wanahabari, Diwani wa Kata ya Chang’ombe, Bakari Fundikila alisema kuwa
ujenzi wa kituo hicho uliogharimu zaidi ya shilingi Milioni 500 umekuwa na
msaada mkubwa kwa wakazi wa kata hiyo. Kituo hicho ni msaada pia kwa wananchi
wa maeneo ya pembezoni kwakuwa awali walikuwa wanatembea umbali mrefu kutafuta
huduma za kiafya.
Diwani Fundikila alisema kuwa kwasasa
kituo hicho kinaendelea kutoa huduma mbalimbali za kawaida na za kibingwa kwa
wananchi. Alisema kuwa kabla ya ujenzi wa kituo hicho huduma hizo walikuwa
wakizifuata katika hospitali kubwa zilizo mbali ikiwemo Hospitali ya Mkoa wa
Dodoma.
“Ukienda kutazama taarifa za
wagonjwa, utakuta kwa siku kituo hiki kinahudumia wagonjwa zaidi ya 200. Kwetu
sisi ni jambo la kushukuru sana kwa kujengewa kituo hiki cha afya” alisema Diwani
Fundikila.
Aidha, alizitaja baadhi ya huduma za
kibingwa zinazotolewa kituoni hapo kuwa ni matibabu ya meno pamoja na huduma za
uzazi kwa wanawake ambazo awali hazikuwepo. Hivyo, alitoa rai kwa wananchi
kufika na kupata huduma kituoni hapo.
Kwa upande mwingine Diwani Fundikila
alimshukuru Rais, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa kutoa fedha, shilingi Milioni 265 katika kukamilisha ujenzi wa Kituo cha
Polisi cha daraja “C” kinachojengwa katika Kata ya Chang’ombe.
“Awali, wazo la ujenzi wa kituo hiki
cha Polisi kiliibuliwa na wananchi na ndipo walianza kukijenga na baadae
tulipoomba fedha serikalini, takapatiwa kiasi cha shilingi Milioni 265 ili
kuhakikisha ujenzi huu unakamilika na matengemeo yetu, mpaka ifikapo mwishoni
mwa mwaka kitakuwa kimekamilika” alisema Diwani Fundikila.
Akihitimisha mahojiano yake na
wanahabari alitoa rai kwa wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anazozifanya katika ujenzi wa miradi na
uboreshaji wa huduma mbalimbali kwa kutunza miundombinu hiyo ili itumike kwa
muda mrefu.
Nae, Gerald Pater, Mkazi wa Kata ya
Chang’ombe aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa ujenzi wa kituo cha afya na
kusema kuwa atahakikisha anatoa elimu kwa wananchi wenzake kuhusu jitihada hizo.
Alisema pia ili kituo hicho kidumu ni wajibu wa kila mwananchi kukitunza.
“Kwa upande wangu nafurahia ujenzi
huu wa Kituo cha Afya Chang’ombe kwa kuwa hadi sasa kimeturahisishia wananchi
kupata huduma za kiafya kwa haraka na wepesi ukilinganisha na hali iliyokuwa
awali” alisema Grace Chatanda Mkazi wa Chang’ombe.
MWISHO
Comments
Post a Comment