Jiji la Dodoma lavuka lengo na kukusanya 103% makusanyo ya mapato ya ndani 2023/2024
Na. Dennis Gondwe, DODOMA
HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imefanikiwa kukusanya
fedha za mapato ya ndani shilingi 51,402,342,226 sawa na asilimia 103 ya lengo
la mwaka wa fedha 2023/2024 wakati ikipeleka fedha nyingi kwenye miradi ya
maendeleo.
Katibu wa Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa Mkutano wa Baraza la
Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo wakati wa Mkutano wa Baraza
la Madiwani wa kupokea na kujadili taarifa za utendaji kazi kwa kipindi cha
robo ya nne (Aprili-Juni, 2024) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri
ya Jiji la Dodoma.
Kayombo ambae ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la
Dodoma alisema kuwa bajeti ya mapato ya ndani ya mwaka 2023/2024 ilikuwa
shilingi 50,097,458,280. Fedha iliyokusanywa ni shilingi 51,402,342,226 sawa na
asilimia 103. Alisema kati ya fedha hizo za mapato ya ndani, asilimia 73.4
ilipelekwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo na asilimia 26.6 ikienda
kwenye matumizi mengineyo.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Kayombo alilipongeza
Baraza la Madiwani kwa kutenga na kutoa fedha za fidia. “Mheshimiwa mwenyekiti,
nilipongeze Baraza la Madiwani kwa kutenga na kutoa fedha. Wananchi 357
wamelipwa fidia ndani ya kipindi cha miezi sita kiasi cha shilingi bilioni 3.2
kati ya shilingi bilioni 3.4 zilizotengwa. Hatuna upungufu wa kulipa fidia, ni
maelekezo ya Chama Cha Mapindzi ngazi ya wilaya na mkoa” alisema Kayombo kwa
kujiamini.
Wakati huohuo, aliutaarifu mkutano huo kuwa
halmashauri imenunua magari mawili kwa ajili ya kusafisha barabara. Alisema
kuwa gari moja lina uwezo wa kufagia barabara kisha mchanga unaofagiliwa
ukafyonzwa. Gari la pili linauwezo wa kudeki barabara kwa presha ya maji.
Alisema kuwa magari hayo yamenunuliwa kwa mapato ya ndani ya Halmashauri ya
Jiji la Dodoma.
Diwani wa Kata ya Tambukareli Juma Michael akifafanua jambo
Nae Diwani wa Kata ya Tambukareli Juma Michael alitoa
rai kwa wananchi kuendelea kulipa kodi na ushuru wa serikali kwa hiari. “Napenda
kuwasisitiza wananchi kuendelea kulipa kodi na ushuru wa serikali kwa hiari kwa
sababu miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika kata zetu inatokana na kodi.
Hivyo, kodi unayolipa ndiyo inayorudi kukuletea maendeleo” alisisitiza Michael.
Ikumbukwe kuwa mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya
Jiji la Dodoma ilikusanya asilimia 80.6 ya mapato ya ndani.
MWISHO
Comments
Post a Comment