Kituo cha Afya Ilazo mkombozi kwa wananchi

 

Na. Mwandishi wetu

MRADI wa ujenzi wa Kituo cha Afya Ilazo utakapokamilika utahudumia wananchi 99,743 wa Kata ya Nzuguni na maeneo ya jirani ikiwa ni mkakati wa serikali ya awamu ya sita wa kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alipokuwa akisoma taarifa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Ilazo kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024.

Dkt. Method alisema kuwa lengo la mradi huo ni kuboresha huduma za mama na mtoto na huduma za upasuaji ukitarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 99,743 wa Kata ya Nzuguni, Ipagala na maeneo menginge watapata huduma bora za afya mradi huo utakapokamilika.

Akiongelea mafanikio ya mradi huo, aliyataja kuwa ni kuwezesha kutoa huduma za upasuaji, kliniki ya mama na mtoto, huduma za kujifungua, wodi ya watoto wachanga, huduma za kuhifadhi miili. Mafanikio mengine ni “wodi hizi pia zimeunganishwa na mifumo ya hewa ya Oksijeni ambayo iko katika wodi ya wazazi, watoto na jengo la upasuaji. Mifumo hii itasaidia wagonjwa wote wenye changamoto ya upumuaji kupata huduma hapa kituoni.  Aidha, huduma za lishe zitatolewa ikiwemo elimu juu ya masuala ya lishe, upimaji wa hali za lishe na ushauri” alisema Dkt. Method.

Kuhusu gharama za mradi huo, alizitaja kuwa ni shilingi 3,094,983,663.32. Kati ya fedha hizo shilingi 2,870,483,663.32 ni gharama za ujenzi na shilingi 224,500,000.00 ni kwa ajili ya Mshauri Mwelekezi na hadi hatua hii iliyofikia kiasi cha shilingi 2,583,435,296.98 kimetumika, aliongeza.

Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Ilazo ulianza kutekelezwa tarehe 04 Julai, 2023 na Mkandarasi Kampuni ya Salem Construction Ltd ya S.L.P 38160 Dar es Salaam na Mshauri Mwelekezi ni Inter Consut Ltd wa S.L.P 423 Dar es Salaam chini ya ufadhili wa KOICA kupitia shirika la kuhudumia watoto UNICEF. Mradi huu unatekelezwa kwa muda wa miezi (13) na unatarajiwa kukamilika tarehe 31 Desemba, 2024.

MWISHO

 

Comments

Popular Posts

Wananchi Makutupora wafunguka changamoto ya Maji, Umeme na Shule kwa Mkuu wa Mkoa

Waziri Mchengerwa apongeza usimamizi wa miradi jijini Dodoma

Mkataba ujenzi Uwanja wa Mpira wa Miguu wasainiwa Dodoma