Msalato washauriwa kuwekeza kwenye Lishe ya watoto
Na. Dennis Gondwe, MSALATO
WAKAZI
wa Kata ya Msalato wametakiwa kuwajenga watoto kiafya kwa kuwaandalia lishe
bora ili kujenga taifa imara lenye uwezo wa kifikra na uchapaji kazi kwa ajili
ya kuliletea maendeleo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Dodoma, Mwl. Neema Majula
Kauli
hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania wa Chama Cha
Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Dodoma, Mwl. Neema Majula alipokuwa akiongea wakazi wa Kata
ya Msalato kwenye maadhimisho ya kuelekea siku ya wanawake duninia ngazi ya
kata yaliyofanyika katika Zahanati ya Msalato iliyopo Halmashauri ya Jiji la
Dodoma.
Mwl.
Majula alisema “ndugu zangu hali ya lishe ni muhimu sana kwa watoto wetu.
Tunapoanza kuwajenga watoto hawa wadogo wawe na lishe bora ndiyo tunajenga
kizazi bora cha taifa hili. Tunakuwa tunawekeza kwenye afya na akili za watoto
ambao baadae wanapoendelea kukua watakuwa wachapa kazi na wenye uwezo mzuri wa
fikra na hivyo, kujiletea maendeleo yao na maendeleo ya taifa letu”.
Akiongelea
maadhimisho ya kuelekea kilele cha siku ya wanawake duniani, alisema kuwa
yanalenga kumhamasisha mwanamke kuchukua hatua kubwa zaidi ya kimaendeleo
kuanzia kisiasa, kijamii hadi kiuchumi.
“Hakuna
maendeleo yoyote yatafanyika bila kuwa na afya njema. Tukijenga jamii yenye
afya nzuri ndiyo, jamii itaweza kufanya shughuli za maendeleo. Kuanzia kwa
watoto wetu ili wasipate udumavu, ili wasipate utapiamlo tukianza kuwanjenga
tangu wakiwa wadogo ili wawe na afya njema ndivyo tunajenga kizazi chenye afya
njema ambacho kitafanya shughuli za maendeleo” alisema Mwl. Majula.

Lishe
ya watoto iende sambamba na lishe ya wababa. “Sasa tujikite kwenye lishe ya
watoto wetu, na mimi nipanua kidogo, jamani mpaka lishe ya wababa pia kina mama
tufanye. Sisi ndiyo waandaaji wa chakula nyumbani tunahitaji kuanadaa lishe
kamili nyumbani, tuweke mchanganyiko wa lishe kamili, wanga, vitamini, protini
ukijenga familia ambayo ina afya njema ndiyo itaweza kuwaza mambo ya maendeleo”
alisisitiza Mwl. Majula.
Kwa
upande wa Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Msalato, Dkt. Abusalami Mpamba alisema
kuwa amefurahishwa na ziara hiyo kujionea utekelezaji kwa vitendo zoezi la
kuwapikia watoto chakula chenye lishe bora. “Mheshimiwa mgeni rasmi, mtoto
ukimlea vizuri akiwa na afya bora ndiyo taifa la kesho. Kwa hiyo, wanawake
waliopata elimu leo itaweza kutusaidia kupata watoto bora na watakaosoma vizuri,
vichwa vyao vitakuwa na akili nzuri kwa sababu wana afya nzuri. Mimi
nikupongeze wewe mgeni rasmi kwa uamizi wako. Umeona tumewaelekeza kwa vitendo
jinsi chakula kinavyoandaliwa, umeona na jinsi wanavyopewa na umeshuhudia
watoto wanavyokula hii ni faraja sana kwetu” alisema Dkt. Mpamba.

Awali
akitoa elimu ya lishe kwa akina mama waliohudhuria kliniki katika zahanati ya
msalato Afisa maendeleo ya jamii kata ya msalato, Alfrida Kitandala alisema
kuwa lishe bora ni muhimu kwa mtoto kwa sababu inamsaidia kuwa na uwezo mzuri
wa kufikiri.
“Kina
mama nawahusia juu ya suala la lishe bora, siyo uji tu kwa mtoto bali ni
mchanganyiko wa vyakula vingi, kuna matunda, kuna madini na vitamini ambazo ni
mboga za majini. Suala la maji ni muhimu kwa watoto wetu, lakini pia kuna
vyakula vya mafuta kama karanga na mafuta tunayotumia. Hivyo, tujitahidi sana
kuzingatia lishe kwa watoto wetu ili iwasaidie hata kufikiria kwao shuleni na
katika maisha ya kawaida” alisema Chitandala.

Nae
mzazi, Jailes Felix alishukuru kwa elimu waliyopewa juu ya lishe kwa watoto.
“Nilikuwa namtania Afisa Afya wa kata kwamba zoezi hili ziwe endelevu
lituhamasishe tuwe tunakuja kliniki mara kwa mara, maana kina mama wengine kuja
kliniki huwa ni nadra sana. Hivyo, Mungu azidi kuwabariki nina hakika tumeelewa
sana kile tulichofundishwa leo na tunakwedna kufanyia kazi” alisema Felix.

Maadhimisho
ya siku ya wanawake Kata ya Msalato yalifanyika kwa kutoa elimu ya lishe bora
kwa wanawake na hamasa ya kujishughulisha yakifanyika katika Zahanati ya Msalato
inayozungukwa na mitaa sita ikikadiriwa kuhudumia watu 11,000.
MWISHO
Comments
Post a Comment