Msalato wamshukuru Rais, Dkt. Samia ujenzi wa shule
Na. Dennis Gondwe, MSALATO
WANANCHI
wa Kata ya Msalato iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamemshukuru Rais wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea shule mpya na kuwapunguzia
wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu.

Afisa Mtendaji Kata ya Msalato, Devotha Selufara akimuelezea Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alichoifanyia Kata ya Msalato
Shukrani
hizo zilitolewa na Afisa Mtendaji Kata ya Msalato, Devotha Selufara alipokuwa
akiwatambulisha wataalam wa kata yake katika Shule ya Msingi Chikole kwa mgeni rasmi Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) Mkoa wa Dodoma.
Selufara
alisema “Shule ya Msingi Chikole ina wanafunzi 790 ilianza mwaka jana mwezi
Julai. Baada ya kumaliza ujenzi ulioanza mwezi Aprili, 2023 kwa fedha ya mama
Samia Suluhu Hassan aliyotupatia shilingi 318,800,000 kwa ajili ya ujenzi wa
shule mpya ya msingi Chikole, ambapo tulijenga madarasa tisa, matundu 16 ya
vyoo, jengo la utawala moja, tumefanikiwa kujenga madarasa ya chekechea ya
mfano ni kama shule za mchepuo wa kiingereza pamoja na madawati yanayotosheleza
madarasa yote. Cha kufurahisha zaidi serikali yake imetujengea kisima cha maji
chenye thamani ya shilingi 22,500,000, hivyo shule hii ni mahali salama kabisa
kwa watoto wetu. Kwa kuwa umefika hapa kiongozi wetu mkubwa wa kimkoa tunaomba
utufikishie salamu sisi wananchi wa Kata ya Msalato za pongezi kwa kuweza
kutukumbuka kutujengea shule hii na kuwapunguzia wanafunzi wetu kutembea mwendo
mrefu”.
Aliongeza
kuwa Rais, Dkt. Samia alitoa fedha shilingi 680,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa
madarasa saba, mabweni manne na vyoo vyenye matundu 10 katika Shule ya
Sekondari ya wasichana Msalato. “Mheshimiwa mgeni rasmi, mama huyu hakuishia hapo,
alitupatia fedha shilingi 437,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya
msingi Msalato pamoja na madawati yake. Ambapo tulijenga madarasa 12, matundu
12 ya vyoo, ofisi mbili za walimu pamoja na eneo la kunawia mikono” alisema
Selufara.
Afisa
mtendaji huyo aliongeza kuwa walianza kujenga kituo cha afya kwa nguvu za
wananchi zenye thamani ya shilingi 50,000,000 hadi usawa wa lenta. “Serikali ya
mama Samia imetupatia fedha shilingi 30,000,000 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi
wa kituo hicho cha afya. Tunamshukuru sana mama yetu. Vilevile, tumejenga zizi
la ng’ombe kwa shilingi 19,800,000. Kwenye Kata hii ya Msalato. Rais mama Samia
ametoa karibia shilingi bilioni 1.3 kwa mwaka wa fedha 2023/2024” alisema
Selufara.

Akiongelea
zawadi za unga wa mahindi, maji, kalamu, na taulo za kike kwa shule za Kata ya
Msalato alisema ni michango ya wananchi wa Msalato. “Hii ni michango ambayo
tumeshiriki pamoja wanaume na wanawake tumeona tuadhimishe na ninyi watoto wetu
wa shule za msingi na sekondari. Tunawashukuru wote walioguswa afya njema”
alisema Selufara.
Comments
Post a Comment