Mkurugenzi Mkuu Wa VETA Afanya Ziara Ofisi Za VETA Kanda Ya Kati Na Chuo Cha VETA Dodoma
MKURUGENZI
Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Prosper Mgaya
amefanya ziara katika Ofisi za VETA Kanda ya Kati na Chuo cha VETA Dodoma
ambapo ametembelea karakana kujionea shughuli za mafunzo na kufanya mazungumzo
na Menejimenti ya Kanda na Chuo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Prosper Mgaya akiwa katika Chuo cha VETA Dodoma na Ofisi ya VETA Kanda ya Kati
Akizungumza
wakati wa ziara hiyo leo tarehe 13 Novemba, 2023, Dkt. Mgaya ameainisha
mikakati mbalimbali ya kuboresha utoaji mafunzo ya ufundi stadi nchini ili
kuwanufaisha wananchi wengi zaidi na kuwawezesha kuendesha shughuli za kiuchumi
kwa ufanisi.
Mikakati
hiyo ni pamoja na kuongeza ubunifu kwenye kuandaa kozi za muda mfupi zinazojibu
mahitaji halisi ya jamii, kuboresha vifaa vya utoaji mafunzo vinavyokidhi
ukuaji wa teknolojia na kuhakikisha ubiasharishaji wa vifaa vya kiubunifu
vinavyozalishwa kwenye vyuo vya VETA.
“Ni
lazima tuongeze ubunifu katika kuandaa kozi za muda mfupi kujibu changamoto zinazowakabili
wananchi kwenye shughuli zao za kiuchumi…tunafanya vizuri sana kwenye eneo la
ubunifu lakini changamoto ni namna ya kuhakikisha ubunifu huo unaingia sokoni
hivyo tunahitaji kuweka nguvu katika suala hili,”amesema
Dkt.
Mgaya ameeleza pia umuhimu wa kupata ithibati za kimataifa kwenye mafunzo
yanayotolewa ili kuwezesha wahitimu wa VETA kutambulika kwenye soko la ajira
kimataifa na kusisitiza nia yake ya kuwezesha walimu kupata mafunzo na ujuzi
ndani na nje ya nchi.
Aidha,
Dkt Mgaya ameeleza kuridhishwa na maandalizi yanayofanywa na Kanda ya Kati kwa
ajili kuanza kutoa mafunzo kwenye vyuo vipya vya ufundi stadi vya Wilaya
yanayotarajia kuanza kutolewa mwezi Januari, 2024 na kumuagiza Mkurugenzi wa
Kanda hiyo kushirikisha viongozi wa Wilaya husika katika maandalizi ya kozi
zitakazotolewa kwenye vyuo hivyo.
Ameelekeza
chuo cha VETA Dodoma kuandaa kozi za aina mbalimbali zinazokidhi mahitaji ya
jamii na kuzitangaza ili wananchi wazifahamu na kujitokeza kujiunga na kozi hizo
ili waweze kujipatia ujuzi wa kuendesha shughuli zao za kiuchumi.
Dkt.
Mgaya amesema mikakati hiyo itachangia kufanikisha malengo ya Serikali ya Awamu
ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwapatia watanzania
ujuzi utakaokuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na kwamba VETA inategemewa
kufanikisha malengo hayo.
Awali,
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, Ndg. John Mwanja aliwasilisha taarifa
ya kanda hiyo inayohusisha mikoa ya Dodoma, Singida na Manyara ambapo amesema
Kanda yake imejipanga vyema katika kuhakikisha vyuo vilivyopo kwenye kanda yake
vinatoa mafunzo bora na kufikia wananchi wengi zaidi.
Mkuu
wa Chuo cha VETA Dodoma, Ndg.Stanslaus Ntibara, amesema hadi sasa, chuo chake
kina jumla ya wanafunzi 4350 ambapo 650 ni wa kozi za muda mrefu na 3700 ni wa
kozi za muda mfupi ikiwa ni ongezeko la asilimia 30 kutoka mwaka 2022.
Comments
Post a Comment