Kamati Ya Bunge Ya Mambo Ya Nje, Ulinzi Na Usalama Imeridhika Na Uendeshaji Na Uendelezaji Wa Kiwanda Cha Maji Cha Uhuru Peak
KAMATI ya Bunge ya Mambo
ya Nje, Ulinzi na Usalama imeridhika na uendeshaji na uendelezaji wa Kiwanda
cha maji cha Uhuru Peak kinachoendeshwa na Suma JKT baada ya kuongeza
uzalishaji wa maji.
Hivyo, imeyataka
mashirika ya umma, Wizara na taasisi za serikali zinunue maji ya Uhuru Peak ili
kuendeleza ukuaji wa kiwanda hicho.
Akizungumza leo
walipotembelea kiwanda hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na
Usalama ya Bunge la Tanzania Vita Kawawa amesema maagizo ya serikali
yalielekeza taasisi za serikali wanapoandaa shughuli mbalimbali wanunue maji
yanayozalishwa na Suma JKT.
Amesema hapo awali
kiwanda hicho kilikuwa kinazalisha lita 250 kwa saa na baada ya kufunga mitambo
mipya yenye uwezo mkubwa wanazalisha lita 10,000 kwa saa na wamebadili
muonekano wa chupa.
"Wameongeza ufanisi
mkubwa ambao tumeshuhudia wenyewe kwani uwekezaji walioufanya kununua kiwanda
kipya umegharimu Sh bilioni 100.6 na kuzalisha maji lita 4,000 kwa saa," amesema
Kawawa
Ameongeza kuwa maji yapo
na yanazalishwa kwa wingi ambayo yana viwango vya kutosha.
Kawawa amesema kazi
iliyopo ni kutafuta masoko ili kufika katika mikoa yote kwani wamewekeza
kibiashara hivyo, watengeneze miundombinu ya kufikia wateja wote
waliowakusudia.
Kwa upande wake, Mkuu wa
JKT, Meja Jenerali Rajab Mabele amesema kamati hiyo ilishinikiza utekelezaji
kwa kupanua kiwanda na kufunga mitambo Ili kuzalisha maji kwa wingi.
Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajab Mabele akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea Kiwanda cha Maji cha Uhuru Peak kilichopo JKT Mgulani jijini Dar es Salaam
"Wameridhika na kile
ambacho waliagiza na tumetekeleza. Niwathibitishie watanzania kwamba
tunadhamira ya kufanya biashara hii ya maji kwani ni salama," amesema Meja
Jenerali Mabele.
Ameeleza kuwa mpango wao
ni kuhakikisha maji hayo yanafika mikoa yote ya Tanzania.
Amesema tayari wameingia
mkataba na Shirika la Reli Tanzania kwa mikoa yote inayopitiwa na reli ya kati
iweze kusafirisha maji yao kwa gharama ile ile ili kutokuwa na utofauti wa bei
kwa watu wa Morogoro na Kigoma.
"Tayari tumefanya
majaribio wametusafidishia maji mpaka Dodoma na biashara ilikuwa nzuri bila
shida yoyote lakini pia tutaongeza magari kwenda zaidi mikoani badala ya Dar es
Salaam pekee," ameeleza.
Comments
Post a Comment