Naibu Waziri Nderiananga ateta na Wanafunzi wa Weruweru
Na. Mwandishi Wetu- Moshi
Naibu Waziri Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Ummy
Nderiananga awaasa vijana kujikinga na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI ili
kuyafikia malengo waliyonayo.
![]() |
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe.Ummy Nderiananga akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Weruweru alipowatembelea shule hiyo |
Kauli hiyo ameitoa
wakati akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Weruweru alipotembelea
mapema Julai 16, 2023 shuleni hapo kwa lengo la kuwapa hamasa wanafunzi wa
shule hiyo ambayo aliwahi kusoma na kutoa zawadi za taulo za kike na mafuta ya
ngozi kwa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi ikiwa ni sehemu ya shukrani kwa
uongozi wa shule hiyo.
Mhe. Nderiananga
aliwaeleza upo umuhimu wa kuendelea kuchukua tahadhari za masuala yanayohusu
Virusi vya UKIMWI kwani kwa mujibu wa tafiti za viashiria vya VVU na UKIMIWI
mwaka 2016/17 zinaonesha kuwa asilimia kubwa ya maambukizi ipo kwa vijana
mwenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 hivyo ipo haja ya kuendelea kuwa makini.
Alitumia fursa hiyo
kuwahimiza kujikinga na mimba za utotoni na kutokatishwa tamaa juu ya ndoto
zao.
"Katika maisha
kukatishwa tamaa kupo, lakini kuwa imara hadi wakatisha tamaa wakate tamaa
wenyewe, hivyo wanafunzi wa Weruweru muwe imara, majasiri na hakika jitihada
zenu hazitapotea bure," alisema
Sambamba na hilo
aliwatoa wasiwasi wanafunzi wa kidato cha sita kuhusu kuendelea na elimu
ya juu kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan imetenga bajeti ya kutosha katika sekta ya elimu kwa ajili ya
kuwawezesha mikopo ya Elimu ya juu.
"Jukumu lenu
kubwa ni kuongeza bidii, nidhamu na weledi katika masomo yenu ili kupata fursa
ya kuendelea na masoma ya elimu ya juu kisha kuzifikia ndoto mlizo nazo,"
alisisitiza Mhe Nderiananga
Kwa Upande wake Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Mwitikio wa Taifa TACAIDS, Bi.Audrey Ngelekela
aliwakumbusha kuendelea kuwa makini kujiepusha na mitandao ya ngono pamoja na
kuchukua tahadhari ili kujiepusha na maambukizi ya VVU na UKIMWI.
Alieleza kuwa,
Serikali kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini imejipanga kuendelea kutoa
elimu kwa jamii hasa vijana ambao ndio kundi linaloathiriwa zaidi na
maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa mwaka
2016/17.
Naye Mratibu wa UKIMWI
wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Dkt. Didas Constantine aliwakumbusha
wanafunzi umuhimu wa kupima afya zao kwa lengo la kujua hali zao za maambukizi
iwapo unagundulika kuwa maambukizi inashauriwa kuanza dawa mapema.
Awali akizungumza
kuhusu shule ya Weruweru mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bi.Rozalia Frimin
alimshukuru Naibu waziri kwa ziara yake shule hapo pamoja na kuwapa zawadi ya
taulo za kike pamoja na mafuta kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi
ikiwa ni sehemu ya shukrani yake kwa mchango wa shule hiyo katika maisha yake.
"Mhe Naibu Waziri
tunakushukuru kututembelea leo, hii imetupa hamasa zaidi sisi na wanafunzi wetu
kwa kuwa umetambua mchango wa shule ya Weruweru, sisi tutaendelea kuunga mkono
jitihada za Serikali kwa kuzalisha vijana wasomi na wenye maadili mazuri
nchini," alisema Mwalimu Frimin.
= MWISHO=
Comments
Post a Comment