Jiji la Dodoma lapewa angalizo lishe bora kwa wananchi
Na. Nancy Kivuyo, DODOMA
Katibu Tawala Mkoa wa
Singida, ametembelea banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuelezwa
shughuli zinazotolewa katika banda hilo kwa upande wa Divisheni ya Kilimo Mjini.
Alielezwa kuwa Kilimo Mjini kinahusiana na kilimo cha kisasa kinachojikita katika mbogamboga na matunda kutokana na ufinyu wa maeneo ya mjini wanapoishi wakulima.
Afisa Kilimo katika Halmashauri
ya Jiji la Dodoma, Athumani Mpanda alieleza kuwa wakulima wanapaswa kutumia
maeneo yao madogo waliyonayo kwaajili ya bustani kiroba. “Hizi bustani kiroba
tunazitumia kupanda mbogamboga ambazo familia itatumia na hii ni kwasababu kama
una kiroba cha kustawisha maua ambayo huyatumii ni vizuri kutumia kuotesha
mboga mboga ambazo zitajumuisha lishe na kupendezesha mazingira yetu” alisema
Mpanda.
Aliongeza kuwa elimu ya
bustani za majumbani imeendelea kutolewa katika taasisi nyingi za serikali pamoja
na shule za msingi na sekondari. “Tumeanzisha elimu hii kwa lengo la
kuhakikisha wakulima na wale wapenzi wa mboga mboga wanapata lishe bora. Hadi
sasa tumefikia asilimia 50 ya kaya zote za Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika
kuwapelekea elimu hii. Kila mwaka tuna mpango wa kutoa elimu ya lishe majumbani
kupitia vikundi, taasisi na hata wakulima wa kaya moja moja. Lakini pia tuna
programu maalum ya uendelezaji wa lishe kwenye jamii inayofanyika kila mwaka”
aliongeza Mpanda.
Nae, Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga baada ya kusikiliza maelezo hayo alisema kuwa sekta ya kilimo inapaswa kuwekewa mkakati madhubuti wa kuhakikisha mazao yanayolimwa yanatoa lishe bora kwa walaji.
Aliongeza kuwa umakini
unahitajika katika usimamizi wa sekta ya kilimo. “Kilimo mjini ndio habari ya
mjini kwasasa, sekta hii inahitaji kuangalia kwa karibu kilimo hiki
kilichogeuka biashara, wapo watu hawazingatii utaratibu wa namna ya kulima na
badala yake wanalima katika mazingira machafu ambayo yanapelekea mbogamboga na
matunda kukuwa katika uchafu na kubeba vimelea vya maradhi. Kwa maana hiyo
muangalie hilo na kuhakikisha mnawakagua na kutoa elimu ya kutosha” aliongeza Dkt.
Mganga.
Banda la Halmashauri ya Jiji
la Dodoma pamoja na seksheni za kilimo, mifugo na uvuvi zinatoa huduma
mbalimbali ikiwemo elimu ya teknlojia ya kilimo, ufugaji na uvuvi, uuzaji wa
viwanja vya matumizi mbalimbali, elimu ya mikopo ya asilimia 10, elimu ya lishe
bora, elimu ya unyonyeshaji maziwa ya mama, elimu ya umuhimu wa Leseni ya
Biashara na ukataji wa leseni ya Biashara na fursa za uwekezaji zilizopo katika
Jiji la Dodoma.
MWISHO
Comments
Post a Comment