Wenyeviti Serikali za Mitaa Hombolo Bwawani wapewa mafunzo huduma ndogo za kifedha
Na. Rehema Kiyumbi, HOMBOLO BWAWANI
Dawati la Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi Halmashauri ya Jiji la Dodoma latoa elimu kwa wananchi wa Kata ya
Hombolo Bwawani juu ya matumizi ya fedha na kuweka akiba kwa lengo la
kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza na wananchi wa kata hiyo,
Mratibu wa Dawati la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Halmashauri ya Jiji la
Dodoma, Hidaya Abdallah alisema kuwa elimu ya huduma za kifedha ni muhimu kwa
wananchi ili kuweza kufahamu namna ya kufanya matumizi na kuweka akiba.
Alisema kuwa kikao hicho
kimewahusisha wenyeviti wa serikali za mitaa kwasababu ndio viongozi wa karibu
na wananchi. “Hii elimu ya huduma za fedha, tunayowaletea ni mahsusi kwenu
kwasababu itawasaidia kufanya maamuzi sahihi wakati wa matumizi. Lakini pia,
katika kutunza na kuweka akiba. Huduma ndogo za mikopo ya fedha, mikopo ya vitu
na vifaa mbalimbali, mikopo ya nyumba, elimu ya ujasiriamali pamoja na huduma
za bima ya afya na bima ya mali ni muhimu kufahamu ili kuwa katika mazingira
salama ya kupata au kutoa huduma bora muda wote” alisema Abdallah.
Aliendelea kusema kuwa katika eneo la sera, sheria na kanuni za huduma ndogo za fedha kuna umuhimu wa wananchi kuzifahamu huku akitaja kuwa benki, wakopeshaji binafsi, watoa huduma ndogo za fedha kwa njia ya kidigitali, vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (SACCOS) na vikundi vya kijamii kama VSL, SILC na VICOBA ni moja ya watoa huduma ndogo za fedha wanaweza kuwatumia ili kukuza uchumi na biashara zao.
Akizungumza katika kikao hicho, alisema kuwa moja ya umuhimu wa sera hizo ni kumlinda mtumiaji na kuwawezesha wananchi kujiwekea akiba na kupata mikopo nafuu kwa ajili ya kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kujikwamua na umasikini.
Aliongeza kuwa pamoja na uwezeshaji
bado kuna changamoto wanakutana nazo. “Hata hivyo, mbali na uwezeshaji na
usajili kutoka kwa wawezeshaji, bado kumekuwa na changamoto katika usajili kwa
wananchi kuwa na hofu ya kupoteza mapato hali inayopelekea kupotea kwa uhuru wa
kujiendesha kwa baadhi ya vikundi kuona kuwa kusajiliwa kutawalazimisha kufuata
masharti ya serikali na kupoteza uhuru wao wa ndani. Naendelea kuwaasa ninyi
viongozi na maafisa maendeleo kuendelea kuwapa elimu wananchi na kuwasilisha
chagamoto zao ili ziweze kutatuliwa” aliongeza Abdallah.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Msisi, Yoram
Magomba alieleza faida alizopata kwenye mafunzo hayo. “Nashukuru sana kupata
mafunzo haya, nikitoka hapa nitaenda kuwaelimisha na wananchi wenzangu ili sote
tuweze kuwa na nidhamu ya fedha. Faida ya kusajili vikundi itaenda kuwa chachu
ya vikundi kufanya vizuri katika matumizi na kutunza fedha” alisema Magomba.
MWISHO
Imehaririwa na Nancy Kivuyo
Comments
Post a Comment