Afisa Biashara Jiji la Dodoma aelezea umuhimu wa kuanzisha Kanda za Huduma
Na. Ramla Makamba, HOMBOLO BWAWANI
Katika kuhakikisha huduma za mapato zinapatikana kwa urahisi na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato halmashauri ya Jiji la Dodoma imeanzisha mfumo wa kanda zitakazohudumia wakazi wa kata mbalimbali kwa karibu ambapo wataalamu watakuwa katika maeneo mbalimbali kutoa huduma hizo zikiwemo huduma za ukataji wa leseni ambapo mpango huo utaanza mapema mwezi Agosti, 2025.
Wananchi watapata huduma kama vile za ulipaji wa tozo mbalimbali katika maeneo yao bila kulazimika kufuata huduma Katikati ya jiji ikiwa ni miongoni mwa harakati za kutatua changamoto za umbali wa upatikanaji wa huduma pamoja na kuhakikisha ukusanyaji thabiti wa mapato ya serikali ambapo mwanzoni yalikuwa hayafanywi kikamilifu.
Hayo
yalisemwa na Afisa Biashara wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Fikiri Mtoi,
katika kikao kilichofanyika Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo Bwawani jengo la
utawala, na kuhudhuriwa na watendaji wa kata, watendaji wa mitaa, wenyeviti wa mitaa
na wadau wa biashara.
Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Biashara wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma aliwaasa watendaji, wenyekiti na wadau wa biashara kuwahamasisha wakazi wa kata zao kutumia na kupokea mpango wa kanda ili kupunguza changamoto katika utoaji wa huduma mbalimbali. Pia wataalamu kufanya kazi zao kwa uwadilifu. “Lengo la kikao hiki ni kutoa elimu ya kuwawezesha watendaji na wenyeviti kuwa na uwezo wa kuwaelimisha wananchi jinsi Halmashauri
ya Jiji la Dodoma ilivyojipanga kuongeza mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026. Pia, kutekeleza majukumu ya ukusanyaji wa tozo kwa kuunda kanda mbalimabali ambazo zitakuwa na wataalamu ambao watashughulika na utoaji huduma kwa wananchi na kutatua kero za wananchi’’, alisema Mtoi.
Aidha, Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Msisi, Rehema Salum alieleza namna alivyonufaika na kikao hicho na mbinu atakazozitumia kuwaelimisha wakazi wa Mtaa wa Msisi. “Katika kikao hiki nimejifunza umuhimu wa kusajili biashara na nitawahamasisha wakazi wa Mtaa Msisi wasiogope na wajitokeze kwa wingi kusajili biashara kupitia huduma za kanda zitakazoanza kutolewa’’ alisema Salum.
Comments
Post a Comment