‘Team Aprili’ wapanda miti Shule ya Msingi Mahungu kusherehekea siku yao ya kuzaliwa
Na. Nancy Kivuyo, KIZOTA
Watumishi
kutoka taasisi mbalimbali za Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamejumuika pamoja
kusherehekea mwezi wa kuzaliwa kwa kupanda miti katika Shule ya Msingi Mahungu.
Wakitoa hisia zao za furaha walipotembelea shule hiyo mpya, watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma akiwemo Afisa Elimu Kata ya Kiwanja cha Ndege, Mwl. Prisca Mgalula alisema kuwa wameichagua Shule ya Msingi Mahungu ili kuongeza uzuri wa mandhari ya shule hiyo mpya. “Mimi nimezaliwa tarehe 26 Aprili na tumeichagua shule hii kusherehekea kwa kupanda miti takribani 100. Kwa maana hiyo tunaendelea kuhamasisha agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dodoma la ‘Mti wangu, Birthday yangu’ kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kutunza mazingira, lakini pia itawasaidia kujifunzia kwa vitendo hapo baadae" alisema Mwl. Mgalula.
Nae,
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mahungu, Onesphory Massawe alianza kwa kusema
kuwa wanafurahi kuwapokea watumushi hao na wanaahidi kuitunza miti hiyo ili
ipendezeshe mandhari ya eneo lote la shule. “Nimpongeze mlezi wetu Afisa Elimu Awali
na Msingi, Madam Prisca Myalla kwa kusimamia vema ujenzi wa shule hii.
Miundombinu yake ni mizuri na itasaidia wanafunzi kujifunza na kufanya vema
katika masomo yao. Tunawashukuru watumishi kwa kutuletea miti hii, tunaahidi
kuitunza na mtakaporudi wakati mwingine mtajionea mandhari mazuri sana” alisema
Mwl. Massawe.
Kwa upande mwingine Mwalimu wa Taaluma, Hadija Nasibu alisema kuwa amefurahia zoezi hilo la upandaji wa miti shuleni hapo. “Tumefurahishwa sana na zoezi hili, watumishi wa Jiji la Dodoma mmefanya jambo jema kuona kwamba mazingira yetu yanafaa kupendezeshwa. Miti hii tutaitunza kwa kuimwagilia maji ili iweze kuleta kivuli. Pia uwepo wa mazingira mazuri utachangia ufaulu mzuri wa wanafunzi” alisema Mwl. Nasibu.
MWISHO
Comments
Post a Comment